Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akisalimiana na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Rais Mstaafu wa
awamu ya nne, Jakaya Kikwete, akisalimiana na Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la klabu ya Yanga na Mke wa
Rais wa Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Fatma Karume,
katika hafla ya kuchangia klabu ya
Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akimsikiliza na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete, katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. Katikati ni Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Dkt.
Harison Mwakyembe. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Rais Mstaafu, Jakaya
Kikwete, akizungumza na Wanachama na wapenzi wa Yanga katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na Wanachama na wapenzi wa Yanga katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akikabidhi mchango wa shilingi milioni 10, kwa Mwenyekiti wa Yanga,
Dkt. Msolla katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond
Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akipokea jezi ya Yanga, kutoka kwa Mbunge wa Iramba Magharibi,
Mwiguru Nchemba,
katika hafla ya kuchangia klabu ya
Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, Juni 15.2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Dar es Salaam, Tanzania
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa amevitaka vilabu vya soka nchini kutumia vema
fursa ya kuwa na mashabiki wengi katika kuvifanya viweze kujitegemea
kiuchumi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Juni 15, 2019) katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.Ameichangia klabu hiyo sh. milioni 10.
“Natambua
kwamba Yanga ni klabu kubwa na kongwe nchini ikiwemo Simba Sport Club
ambazo ndizo zina wanachama na mashabiki wasiopungua milioni 20 au
zaidi.”
Hivyo,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuvitaka vilabu vya soka nchini
kutafuta njia nzuri na endelevu ya kupata mapato ili kuendesha timu zao
na kujiimarisha kiuchumi.
Amesema
kwamba, kuimarika kwa vilabu hivyo vyenye ushawishi mkubwa katika soka
nchini ni muhimu kwa mustakabali wa soka la Taifa letu.
Waziri
Mkuu amesema kufanya vizuri kwa vilabu hivyo kuna uhusiano wa mkubwa na
wa moja kwa moja na mafanikio ya timu ya soka ya Taifa.
“Nampongeza
kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kwa kazi nzuri aliyoifanya msimu ulioisha
na kuiwezesha timu ya Yanga kufanya vizuri ingawa haikupata ubingwa.”
Pia,
Waziri Mkuu amesema yeye ni mpenzi wa timu zote zinazoshinda na
zinazoshindwa. “Kama kuna timu naipenda sana ni siri yangu, hata nyie
hamuijui.”
Waziri
Mkuu amesema soka ni mchezo maarufu na una wapenzi wengi duniani na
hapa nchini na umejipambanua kwa fursa nyingi ikiwemo biashara,
uwekezaji na ajira.
Amesema
Serikali imeendelea kusimamia maendeleo ya michezo, ukiwemo mchezo wa
soka ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka
2015-2020.
“Mhe.
Rais Dkt. John Magufuli amekuwa akiungana na wanamichezo kuhamasisha
kuendeleza michezo na anatamani kuona mkishinda hadi katika ngazi ya
Afrika.”
Kadhalika,
Waziri Mkuu amezipongeza timu zote za soka zinazofanya vizuri katika
ngazi mbalimbali. “Tumeshuhudia Polisi na Namungo FC zikipanda hadi ligi
kuu.”
Ameipongeza
timu ya Simba kuwa klabu bingwa, Azam kuwa bingwa wa FA, Serengeti boys
na Twiga kuliwakilisha Taifa na Taifa Stars inashiriki AFCON – Misri.
“Kitendo
cha Azam kushinda FA na Simba kushiriki vizuri AFCON sasa kumewezesha
timu zetu mbili zaidi, Yanga na KMC kupata nafasi ya kushiriki
mashindano ya CAF.”
Kuhusu
harambee ya Kubwa Kuliko, Waziri Mkuu amesema ni mwanzo mzuri kuelekea
kwenye mabadiliko yatakayoiwezesha Yanga kujitegemea na kujiendesha bila
kutarajia michango kama ilivyo sasa.
Naye,
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amewataka wanachama
wa Yanga warudishe hisia na mapenzi kwa timu yao kama ilivyo kwa timu ya
Simba, pia wawe na ubunifu wa kutengeneza mfumo mzuri wa mapato.” Siku
hizi Yanga imekuwa baridi sana, viongozi wa Yanga lazima mbadishe hali
hii.”
Amesema
viongozi wa sasa wa klabu ya Yanga chini ya Uwenyekiti wa Dkt. Mshindo
Msolla ni wazuri na wanaujua mpira vizuri, hivyo watengeze mifumo mizuri
itakayoinufaisha klabu. Wahakikishe wanawekeza kwenye timu ya watoto
badala ya kuangalia wachezaji wa kutoka nje ya nchi pekee.
Amesema
wasipowekeza kwenye timu ya watoto siku zote watakua mafahari wa kuwa
na wachezaji kutoka nchi za nje jambo ambalo ni sawa na kuwafundishia
wenzao. “Leo mnajisifia na akina Makambo, Kagere siku ikicheza timu ya
Taifa inakuwaje. Oneni fahari ya kuwa na wachezaji wa ndani hivyo
waendelezeni Tanzania kuna vijana wana vipaji.”
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Dkt. Mosolla amesema yeye pamoja na
viongozi wenzake watahakikisha wanajenga umoja ndani ya klabu na
kuipeleka jirani na wananchi kwa kufufua matawi na kuwa na wanachama
wapya wengi.
Pia
watawatumia wachezaji wa zamani katika kupata wanachama wengi na pia
watakuwa na wiki ya klabu hiyo ambayo wataitumia kwa kufanya shughuli
mbalimbali za kijamii na kurudisha utaratibu wa kwenda mikoani baada ya
ligi kuisha kwa ajili ya kutembelea wananchi na kujiongezea wsanachama.
Kuhusu
suala la mabadiliko ya katiba amesema watalifanya kwa kufuata utaratibu
wa kisheria. Pia Dkt. Msolla amesema uongozi wake utahakikisha
unazingatia utawala bora na tayari wametoa matangazo ya nafasi za ajira.
Akizungumza
kuhusu hali ya usajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, amesema
hadi sasa tayari wamekamilisha kwa asilimia 90 kuwasajili wachezaji wote
aliowataka kocha wa timu hiyo Mwinyi Zahera kutoka nje ya nchi na wa
ndani ya nchi.
Dkt.
Msolla ametumia fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu awasaidie ili Serikali
iweze kuwapunguzia changamoto mbalimbali zinazoikabili klabu hiyo ya
Yanga ikiwemo ya madeni.
Awali,Mwenyekiti
wa Kamati ya Hamasa wa klabu ya Yanga, Anthony Mavunde, alisema kamati
hiyo ilikuwa na wajumbe 27 waliofanikisha kupatikana kwa fedha ambazo
zimetumika katika kusajili wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao wa
ligi.
Mavunde
ambaye pia ni Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu,
Bunge, Ajira na Vijana alisema walisambaza kadi kwa ajili ya kukusanya
fedha za kuimarisha klabu yao ili iweze kujiendesha na kutatua
changamoto za wachezaji.
Alisema
mbali na kukusanya michango pia kamati yao imependekeza kufanyika kwa
mabadiliko ya katiba ili kutengeneza mfumo mzuri utakaoisaidia timu hiyo
kuweza kujiendesha na kuweka mfumo mzuri wa kutumia vifaa vya klabu
kukuza uchumi.
Kwa upande wake,
Mjumbe wa Baraza la Wadhamini la klabu ya Yanga na Mke wa Rais wa
Kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Fatma Karume amewataka
wananchi wasitumie vilabu vya soka kama njia ya kutaka kujipatia nafasi
za kisiasa. Pia amewataka wanachama wampe ushirikiano Mwenyekiti wao
mpya.
Naye,
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe
alisema hakuna kipindi kigumu kilichompa tabu katika kuongoza wizara
hiyo kama kipindi ambacho timu ya Yanga ilipokuwa katika mgogoro wa
kiuongozi.
Pia,
Dkt. Mwakyembe alionesha kutoridhishwa na upangwaji wa ratiba za
michezo mbalimbali ya ligi kuu msimu uliopita, hivyo alitumia fursa hiyo
kuwahakikishia wapenzi wa soka nchini kwamba mambo hayo hayatajirudia
tena katika msimu ujao.
No comments:
Post a Comment