Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi
Japhet Maselle (kulia), akikagua kivuko cha MV. Pangani II kilichokuwa
kinafanyiwa ukarabati mkubwa. Kivuko hicho kilihamishwa kutoka Utete Wilaya ya Rufiji
ambapo kilikua kinatoa huduma kati ya Utete na Mkongo katika mto Rufiji.
Kushoto ni Meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina.
ALFRED MGWENO (TEMESA) TANGA
Kivuko cha MV. Pangani II ambacho
awali kilikua kikijulikana kama MV. Utete kinatarajiwa kukamilika hivi karibuni
na kuanza kutoa huduma katika mto Pangani kati ya Pangani na Bweni mkoani Tanga.
Kivuko hicho ambacho kilikuwa kikifanyiwa ukarabati mkubwa kilihamishwa kutoka
Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani kilipokuwa kinatoa huduma kati ya Utete na Mkongo
kutokana na mto Rufiji kukauka maji kwa kiasi kikubwa na kukosa kina na hivyo
kusababisha kivuko kushindwa kufanya kazi kwa kipindi kirefu. Kwa sasa wakazi
wa maeneo hayo wanahudumiwa na boti ya MV.
Mkongo inayobeba abiria arobaini
ambayo ina uwezo wa kutembea kwenye maji mafupi.
Akikagua kivuko hicho mapema leo,
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Mhandisi Japhet Maselle ambaye
aliambatana na Meneja wa TEMESA mkoa wa Tanga Mhandisi Margareth Gina na mkuu
wa kivuko Pangani Bweni Mhandisi Abdulrahman Ameir, aliridhishwa na kazi ya
ukarabati huo, hata hivo aliagiza kazi hiyo ikamilike mapema ili kivuko hicho
kiingizwe kwenye maji tayari kwa kufanyiwa majaribio ya mwisho na kuanza kutoa
huduma.
‘’Baada ya hapa tunatarajia kufanya
ukarabati mdogo wa kivuko cha MV. Tanga ikiwemo kukipaka rangi hivyo basi
hakikisheni mnamaliza kazi hii kwa haraka ili tuweze kukamilisha ukarabati huo
mapema na kuanza kutumia kivuko hiki’’, alisema Mhandisi Maselle.
Aidha Mtendaji mkuu alimuagiza
msimamizi wa matengenezo hayo kuhakikisha anamalizia ukarabati huo kama ambavyo
mkataba unamtaka.
Awali Mhandisi Maselle
alitembelea karakana ya TEMESA mkoa ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na
wafanyakazi na kukagua baadhi ya miundombinu iliyopo katika karakana hiyo ikiwemo
mitambo pamoja na kukagua chumba cha kuhifadhia vipuri vya magari na vifaa vya
matengenezo kinga ambapo aliridhishwa na akiba kubwa ya vipuri iliyoko katika
karakana hiyo na kumpongeza meneja wa mkoa huo kwa kuanza kutekeleza maagizo
ambayo aliyatoa alipotembelea mwishoni mwa mwaka jana. Kuwepo kwa akiba ya
kutosha ya vipuri vinavyotoka kwa haraka huwezesha karakana kutengeneza magari
kwa muda mfupi na kwa uharaka zaidi.
No comments:
Post a Comment