HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 20, 2019

Wafanyabiashara Sethi na Rugemarila waendelea kusota rumande

NA JANETH JOVIN

MMILIKI wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, Habinder Sethi na Mfanyabiashara, James Rugemarila wanaendelea kusota rumande kwa mwaka wa tatu sasa kutokana na upelelezi wa kesi ya utakatishaji fedha inayowakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kutokamilika.

Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa kesi hiyo imekuja kwa ajili ya kutajwa.

Swai alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo aliomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.

Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 4, mwaka huu na washitakiwa wamerudishwa rumande.

Washitakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27 kwa mara ya kwanza walifikishwa mahakamani hapo Juni 19, 2017.

Washitakiwa hao wanadaiwa kuwa Oktoba 18, 2011 na Machi 19 , 2014 jijini Dar es Salaam walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ili kutenda kosa.

Aidha, inadaiwa katika mashitaka ya kujipatia fedha kwamba  kati ya  Novemba 28 na 29, 2011 na Januari 23,2014 katika Makao makuu ya Benki ya Stanbic Kinondoni  na Benki ya Mkombozi tawi la Mtakatifu Joseph,  kwa ulaghai washitakiwa hao walijipatia kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Dola za Marekani  22,198,544.60 na Sh 309, 461,300,158.27. 

Pia washitakiwa wote wanadaiwa kuisababishia serikali hasara ambapo inadaiwa walitenda makosa hayo Novemba 29, 2013 katika Benki ya Stanbic tawi la  kati kinondoni, kwa vitendo vyao waliisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 22, 198, 544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Kati ya Novemba 29,2013 na Januari 23, 2014 maeneo tofauti Dar es Salaam kwa pamoja walitenda kosa la kutakatisha fedha kwa kuchukua fedha kutoka BoT ambazo ni dola za Marekani milioni 22.1 na Sh bilioni 309.4  wakati wakijua fedha hizo ni zao la kujihusisha na genge la uhalifu.

No comments:

Post a Comment

Pages