HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 20, 2019

Waliojifanya maofisa wa Takukuru wafikishwa mahakamani

 Watuhumiwa wa mashitaka matatu likiwamo kujifanya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakiingia mahakamani.

NA JANETH JOVIN

MKUU wa Kitengo cha mauzo cha Ramada Hoteli William Mgatta (36) na wafanyabiashara wawili wamefikishwa katika  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashitaka matatu ikiwemo la Kujifanya maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na kushawishi rushwa ya Sh. Milioni 300.

Mgatta na wenzake wawili ambao ni Mohammed Abdallah (25) na Daniel Ileme (35) wamefikishwa mahakamani hapo leo mchana  na kusomewa mashitaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Maira Kasonde.

Akisoma mashitaka hayo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Aneth Mavika  alidai kuwa katika shtaka la kwanza washtakiwa walijihusisha na vitendo vya rushwa.

Mavika alidai Mei Mosi 2019, na Juni  10, mwaka huo huo, katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na Arusha, mshitakiwa Abdallah na Ileme wakiwa wafanyabiashara na mshtakiwa Mgatta akiwa Mkuu wa Kitengo cha mauzo cha Ramada hoteli walishawishi rushwa ya Sh. Milioni 300 kutoka kwa Francis Matunda kama kishawishi ili wasimchukulie hatua za kisheria kwa kukataa kuwalipa wafanyakazi wake kiasi cha Sh. Bilioni moja.

Pia alidai kuwa kwa tarehe tofauti katika eneo lisilotambulika jijini Dar es Salaam na Arusha washtakiwa Abdallah, Ileme na Mgatta walikula njama ya kutenda kosa la kujifanya ni watumishi wa umma.

Wakili Mavika alidai kuwa katika shtaka la tatu, Juni10, mwaka huu katika eneo lisilojulikana kwa sasa jijini Dar es Salaam na Arusha kwa pamoja washtakiwa hao walijifanya ni watumishi wa Takukuru kitu ambacho walijua kuwa si kweli.

Baada ya maelezo hayo, Wakili Mavika  alidai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa na hawana pingamizi la dhamana endapo washtakiwa watatimiza Masharti.

Akitoa masharti ya dhamana, Hakimu Kasonde alimtaka kila mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja,  kuwalisilisha mahakamani kiasi cha Sh.Milioni 50 au hati ya mali yenye thamani ya fedha hiyo na kusaini bodi ya Sh. Milioni 50.

Hata hivyo washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti hayo, hivyo wamepelekwa rumande kesi imeahirishwa hadi Julai 4, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

Pages