HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 04, 2019

JAMII CHIBUMAGWA YAHAMASISHWA KUACHANA NA NYUMBA ZA TEMBE ILI KUBORESHA MAKAZI

 Mzee Wilfred Nyaombo mkazi  wa Kijiji cha Chibumagwa kilichopo kata ya Sasajila Wilayani Manyoni akishiriki kubeba tofali wakati ya Kampeini ya Kitaifa kuhamasisha wananchi kuboresha makazi yao kampeini inayoendelea kijijini hapo kuhamasisha wananchi kuachana na nyumba za asili zijulikanazo kama Tembe.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu akiongea na wananchi wa Kijiji cha Chibumagwa kilichopo kata ya Sasajila Wilayani Manyoni wakati wa Kampeini ya Kitaifa kuhamasisha wananchi kuboresha makazi kazi inayoendelea katika kijiji hicho kilichopo kata ya Sasajilwa Wilayani Manyoni.

Na Anthony Ishengoma, Singida
 
Wakazi wapatao 5,997 wa Kijiji cha Chibumagwa kilichopo kata ya Sasajila Wilayani Manyoni wanaendelea na uboreshaji wa makazi yao baada ya kupata hamasa kutoka kwa Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii kupitia kampeni yake kitaifa ya kuboresha Makazi na kuachana na nyumba za jadi.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,  Wazee na Watoto Idara Kuu Maendeleo ya Jamii hivi karibuni itazindua kampeni hiyo Kitaifa na kwa kuanzia  imeanza na Chibumagwa kama kijiji cha mfano kwa kuanza na maboresho ya makazi ya nyumba sita za  wazee wasiojiweza na watu wenye mahitaji maalumu kwa kushirikisha wananchi kijijini hapo ili wao kama sehemu ya jamii waone umuhimu wa kujiletea maendeleo kwa kuboresha makazi kwa njia ya kujitolea kwa pamoja.
Akiongea na wakazi wa Kijijini Chibumagwa wilayani Manyoni mkoani Singida Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema kuwa kampeni ya kuboresha makazi bora imeanzia kijijini hapo lakini ni matarajio ya Serikali kuwa kampeini hiyo itaendelea nchini kote na kuwataka wakazi wa kijiji hicho kuachana na nyumba za Tembe na waboreshe makazi ya kwa kutumia nyumba zilizojengwa kwa tofali.
Aidha Katibu Jingu aliongeza kuwa nyumba za Tembe zimekuwa na usumbufu mkubwa kwa kuwa zinatakiwa kufanyiwa maboresho hasa wakati wa kipindi cha mvua jambo ambalo uwafanya wakazi hao kulazimika kujenga kila mwaka kutokana maji ya mvua kuleta usumbufu mkubwa na kusababisha kuwepo kwa ujenzi mpya kila mwaka.
Dkt. Jingu ameyataja madhara mengine ya nyumba za jadi kuwa ni kukosekana kwa hewa ya kutosha ndani ya nyumba hizo, kuwepo kwa wadudu kama vile mijusi na lakini pia kuwa na madhara makubwa kiafya hivyo kuwataka wakazi hao kwapamoja kushirikiana ili kila familia kijijini hapo kuwa na makazi yaliyoboreka.
Akisoma Risala fupi kuhusu kampeni hiyo Kijijini hapo Afisa Mtendaji wa Kijiji hicho Bw. Benjamin Njauka alisema kuwa lengo la kampeni hiyo Kijijini hapo ni kuhamasisha jamii kuboresha makazi kwa mtu mmoja mmoja kwa njia ya kushirikiana akiongeza kuwa jamii hiyo inahamasishwa kwa njia ya mikutano ya hadhara ikiwemo ushauri kutoka kwa viongozi wa dini.
Aidha Bw. Njauka Kijiji chake tayari kimefanikiwa kufyatua tofali 14,553 na kati ya hizo tofali 18,000 hizo zitatumika kujenga nyumba sita za awali na kuhaidi kuwa uifikapo tarehe 6 mwezi huu vitongoji vinavyounda kijji hicho vitakuwa vimekamilisha ufyatuaji tofali na nyumba sita za awali zitakuwa tayari ifikapo Julai 30.    
Wakati huo huo Mkazi wa Kitongoji cha Msakile Kijiji cha Chibumagwa Wilfred Nyaombo alisema kuwa kampeni imepokelewa kijijini hapo kwa mwitikio mkubwa na vijana wamehamasika vya kutosha na kushiriki kikamilifu katika hatua ya wali ya ufyatuaji tofali kwa ajili ya kuanza ujenzi wa nyumba za watu wenye mahitaji maalumu.
Aidha Afisa Ustawi wa Jamii wa Wilaya ya Manyoni Bi. Maua Ngusa amesema mradi wa makazi bora katika Kijiji cha Chibumagwa ni wa mfano na unaanza na kwa wananchi wenye maisha duni kabisa lakini nyumba zitakazo jengwa zitatumika pia kwa watu wengi kuiga ujenzi wake ili kuboresha makazi yao.
Kijiji cha Chibumagwa  na vitongoji vyake vinashiriki katika kampeni hii ambayo ni ya kitaifa yenye kaulimbiu ya piga kazi boresha makazi  na tayari kampeni itaanza na mikoa mitano na moja ya mikoa ya mwanzo ni mkoa Singida pamoja na mkoa wa Geita na inafanyika ili kuwawezesha wananchi kuishi kwenye makazi yaliyobora.

No comments:

Post a Comment

Pages