Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo Profesa Damian
Gabagambi akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani).
Na Janeth Jovin
SHIRIKA la Taifa la Maendeleo (NDC) limesema kuwa limelenga kuondoa jembe la mkono kwa wakulima kwa kuleta mradi wa kuunganisha na kusambaza matrekta nchini.
Mradi huo ambao utawawezesha wakulima watakaofika katika Viwanja vya Maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) kupata treka kwa mkopo kwa kutoa kiasi cha Sh. Milioni tatu kama kianzio kisha fedha zingine kulipa kidogo kidogo mpaka atakapomaliza deni.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika maonesho hayo ya 43 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba), Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Profesa Damian Gabagambi alisema mradi huo ni mpango wa nchi kati ya Tanzania na Poland wenye lengo la kuwasaidia wakulima kwa kuondoa jembe la mkono.
Alisema matreka hayo upatikana kwa mkulima kutoa asilimia 25 ya fedha ambayo trekta linauzwa lakini katika msimu huu wa sabasaba wametoa ofa kwa wananchi kupata mkopo wa matreka kwa masharti nafuu kwa kuanza kutoa kiasi cha Sh.Milioni tatu.
"Katika msimu huu wa sabasaba wananchi wanaohitaji matrekta kwa mkopo wataanza kutoa Milioni tatu na watapatiwa trekta fedha inayobaki watalipa kidogo kidogo ndani ya miaka miwili bila riba isipokuwa atakaposhindwa kulipa ndani ya muda huo atalazimika kulipa kwa riba.
Tunamtaka atakayeomba treka kwanza aende kijijini kwake aandike barua ambayo itadhibitishwa na mtendaji wa kijiji kisha ataipeleka kata ikadhibitishwe na mtendaji wa kata na mwisho atapeleka kwa Mkurugenzi wa halmashauri husika, tunafanya haya yote ili tuweze kupata watu waaminifu wanaohitaji trekta hizi, " alisema.
Aidha alisema wanaendelea kujipanga ili adhma hiyo ya kuondoa jembe la mkono kwa wakulima nchini liweze kutimia.
"Tunataka jembe hili la mkono libaki katika makumbusho ya Taifa kwa sababu tunapoelekea halitakidhi mahitaji, " alisema.
Hata hivyo alisema upande mwingine ambao shirika hilo limejikita ni kwenye dawa ya viwadudu vya kuuwa mazalia ya mbu.
Prof. Gabagambi amesema tayari wameshatoa wito kwa taasisi zote nchini kutumia dawa hizo ambazo zinazalishwa kwa wingi katika kiwanda kilichopo mkoani Pwani.
Alisema tayari kiwanda kinauwezo wa kuzalisha dawa hizo za kukidhi mahitaji ya ndani na kwa ajili ya kusambaza katika bara lote la Afrika.
No comments:
Post a Comment