HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 09, 2019

NEMC: Wataalam elekezi wa mazingira changamkieni maonesho 77

Ofisa  Mazingira wa NEMC, Elias Chundu (kulia), akitoa elimu juu ya utunzaji  wa mazingira kwa wananchi (kushoto) waliotembelea  banda la baraza hilo katika Maonesho  ya 43  ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).
 

Na Mwandishi  Wetu, Dar es Salaam

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limewataka wataalamu elekezi wa mazingira  hapa nchini kutumia fursa ya maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam kukamilisha ada, tozo na michango mbalimbali wanayopaswa kulipia katika kipindi
husika.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dk. Samuel Gwamaka kwenye maonesho yanayoendelea Jijini Dar es Salaam, Mhasibu wa Baraza hilo, Bi. Beatrice Kilimo amesema maonyesho ni fursa pekee kwa watalaamu elekezi kuchangamkia fursa hiyo.

“NEMC tupo kwenye Banda la Katavi  chumba namba 53 na 54 tukiwatumejikita katika kutoa elimu kwa umma kuhusiana mambo mbalimbali yanayohusu uhifadhi na utunzaji wa mazingira na huduma nyinginezo,” Bi. Kilimo alisema.

Alisema  pamoja na mambo mengine wanatumia maonyesho hayo ya  biashara ya kimataifa maarufu kama Sabasaba kupokea tozo mbalimbali  na ada  za mwaka kwa wataalamu elekezi ambao hawajalipa mpaka sasa. 

“Sisi  kama Baraza tumejipanga kutoa elimu endelevu ya mazingira kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo na pia kwenda sambamba na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga uchumi wa kati na viwanda ifikapo mwaka 2025,” alisema Afisa huyo. Bi.  Kilimo  mbali ya kuhamasisha watu na wadau mbalimbali wa mazingira kujitokeza kwa wingi kwenye banda la Baraza, alisema wanasajili pia miradi pamoja  sambamba na utoaji wa risiti na hati za malipo.
“Tupo vizuri na tumeridhishwa na huduma zinazotolewa na waandaji wa maonyesho haya ambao ni Mamlaka ya Maendeleo ya  Biashara Tanzania (TANTRADE) na watu wengi wanakuja kujifunza na elimu juu ya
mazingira,” alisema.

Kwa upande wake mdau wa mazingira, Bw. Paschal Antony, mkazi wa Morogoro aliyetembelea banda la NEMC  amelipongeza Baraza hilo kwa kuwa imara katika kusimamia na kutekeleza Sheria na Kanuni za mazingira kwa vitendo.
“Kumekuwa na mwitikio mkubwa  miongoni mwa watanzania hasa katika suala nzima la uhifadhi na utekelezaji wa mazingira,” alisema na kuishauri NEMC kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwenye shule za msingi na sekondari.
NEMC wameendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kutunza mazingira ambapo nyingi ya hatua hizo zimekuwa zikiungwa mkono na wadau wa mazingira wa ndani na nje ya nchi ikiwemo upigaji marufuku matumizi ya
mifuko ya plastiki ambayo ilikuwa kero kwa ustawi wa mazingira hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages