HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 26, 2019

Benki ya Stanbic yatoa bilioni 177 kuwezesha miundombinu nchini Tanzania

NA MWANDISHI WETU

BENKI ya Stanbic Tanzania imethibitisha dhamira yake ya kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Taarifa ya Benki hiyo kwa vyombo vya habari, imesema kuwa ndani ya mwaka 2019 imetoa billion 177 kufadhili miradi mbalimbali ya miundombinu ikiwemo barabara, maji na umeme.
 
Akizungumza juu ya ufadhili huo, Mkurugenzi Mkuu wa benki ya Stanbic, Ken Cockerill alisema kuwa Benki ya stanbic ina nafasi kubwa katika kuchangia Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP II), unaolenga kuinua ukuwaji wa viwanda na kuleta maendeleo ya jamii na uchumi kwa ujumla,” Cockerill alisemaa.
 
Kwa kuzingatia hilo tunafurahi kuwa mstari wa mbele katika kuziba pengo la ukosefu wa fedha za kuwekeza kwenye miundombinu ambayo ni muhimu katika kuleta maendeleo nchini Tanzania.
 
Uchangiaji wa sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ndio suluhu ya matatizo yanayokabili sekta mbali mbali ikiwemo wafanyabiashara. Uwekezaji huu utachangia katika kuboresha nguvu kazi, pamoja na kukuza uchumi wa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
 
Serikali ya Tanzania imetoa zaidi ya TZS trilioni 12.2 (USD 5.3 billion) kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambayo inahusisha ujenzi wa reli ya Standard Gauge Railway (SGR), bomba la mafuta kutoka Uganda-Tanzania (Crude Oil Pipeline) na ujenzi wa kituo cha 3 cha kisasa katika uwanja wa ndege wa taifa - Julius Nyerere International Airport Terminal 3.
 
Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma za kibenki za Mashirika na Uwekezaji wa Benki ya Stanbic, Manzi Rwegasira alisema “Tanzania iko katika safari ya kuziba pengo la upatikanaji wa miundombinu, jambo ambalo ni ngao katika kufanikisha uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025”.
 
Idadi ya watu nchini Tanzania inakuwa kwa kiwango cha milioni 1.6 kila mwaka na tunakadiria kufikia watu milionii 67 mwaka 2025 na milioni 77 ifikapo mwaka 2030. Hivyo ni muhimu kuwa na miundombinu ya kisasa ambayo itakidhi mahitaji ya watu hao na maendeleo ya kiuchumi. Rwegasira aliongeza kuwa “ushirikiano kati ya sekta binafsi kama benki ya Stanbic na serikali ndio chachu ya maendeleo jumuishi nchini”.
 
Takwimu za mwaka 2018 kutoka Benki ya Tanzania (BoT), zinaonyesha kuwa uchumi wa Tanzania unakuwa kwa kiwango cha asilimia 6.6, hivyo maendeleo ya miundombinu yatachangia moja kwa moja ongezeko la kiwango hicho. Mwaka huu, uchumi unategemewa kukuwa kwa asilimia 7.1 huku miundombinu kama barabara, bandari na reli zikitabiriwa kuongeza pato la taifa kwa kasi.
 
Tangu mwaka 2018 benki ya Stanbic imetoa zaidi ya bilioni 300 kufadhili kampuni mbali mbali za kitanzana katika sekta za kilimo, viwanda, maliasili na taasisi za serikali, Benki hiyo imedhamiria kufanya kazi bega kwa bega na serikali, na wadau muhimu ili kuboresha mazingira ya uwekezaji na kuhakikisha Tanzania inafikia malengo yake ya kuwa uchumi wa kati wa viwanda ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment

Pages