HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 24, 2019

MTOTO WA MKUU WA MAJESHI 'CDF' AFA KATIKA AJALI YA NDEGE


aliyekuwa Rubani wa Ndege iliyoanguka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambaye ni Mtoto wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali, Venance Mabeyo, marehemu Nelson Mabeyo.

Mabaki ya ndege iliyoanguka na kuua watu wawili.



NA GRACE MACHA, ARUSHA

MTOTO wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali, Venance Mabeyo, Nelson Mabeyo amefariki dunia kwenye ajali ya ndege iliyotokea uwanja mdogo wa ndege wa Seronera uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Nelson ambaye alikuwa rubani wa ndege ndogo ya Kampuni ya Auric alipata ajali hiyo jana saa 1.30 asubuhi akiwa na Nelson Orutu ambaye ni rubani mwanafunzi na wote wawili walifariki papohapo.

Ajali hiyo ilitokea wakati marubani hao wakirusha ndege hiyo kuelekea kwenye uwanja mdogo wa Gurumeri uliopo kwenye hifadhi hiyo kwa ajili ya kuchukua watalii waliokuwa wakisafiri kuelekea kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye uwanja wa ndege wa Seronera, Msimamizi wa Kampuni ya Auric, Peter Kimaro, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo.

“Baada ya kuhakiki na kuona ndege iko sawa na kuruhusiwa kuruka kwenda Gurument kuwachukua wageni kuwapeleka KIA, walipoingia na kuondoka na mimi nikajua wako sawa,” alisema Kimaro.

Alisema baada ya kuona ndege imeshika mwendo na kupaa kidogo, ilikata kona badala ya kunyooka, hali ambayo ilimshangaza.

“Baada ya muda mfupi ndege hiyo ikagonga choo cha uwanjani na kuanguka. Wote walifia ndani ya ndege,” alisema.

Alieleza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji walifika eneo la tukio na kuzima moto. Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika Zahanati ya Seronera.

Habari kutoka mamlaka ya viwanja wa ndege imeeleza kuwa Nelson aliondoka na ndege hiyo juzi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.

Mapema jana, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Pascal Shelutete, alithibitisha kutokea ajali hiyo.

"Tunatoa taarifa zaidi baadaye kwani sasa kazi inayoendelea ni kuokoa vitu na kuhifadhi miili," alisema Shelutete.

No comments:

Post a Comment

Pages