HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 06, 2019

Serikali yashauriwa kuangalia Sera ya Afya

NA SULEIMAN MSUYA

SERIKALI imeshauriwa kuangalia upya Sera ya Afya ili kuondoa changamoto ya ucheleweshaji dawa muhimu kwa kina mama wajawazito wakati wa uzazi.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Health Promotion Tanzania (HDT), Mchungaji Dk. Peter Bujari wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Dk.Bujari alisema Sera ya Afya imeweka wazi kuhusu kutokuwepo kodi kwenye dawa muhimu lakini mchakato wa dawa hizo kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD), unakuwa mrefu hali ambayo inachangia vifo vya kina mama.

Alisema utafiti ambao walifanya mwaka 2015/2016 umeonesha wakina mama wengi wanapoteza maisha wakati wa kujifungua kwa kukosa dawa muhimu hivyo serikaki inapaswa kuangalia Sera ya Afya ili isiwe chanzo cha vipo.

Mkurugenzi huyo alisema takwimu zinaonesha wakina 15,017 kati ya 100,000 wanaojifungua wanapoteza maisha kwa mwaka hiyo ikiwa ni sawa na wakina mama 1,250 kwa mwezi na 41 kwa siku.

Alisema utafiti huo umeonesha vifo vingi vya mama wajawazito vinawahusu wasichana wenye umri chini ya miaka 18, waliozaa watoto wengi bila kufuata uzazi wa mpango na upungufu wa damu.

"Tumefanya utafiti wa kutosha na tumejiridhisha kuwa MSD kuchelewa kutoa dawa ni moja ya sababu inayochangia vifo vya kina mama ndio maana tunaomba Sera ya Afya iangaliwe upya ili iweze kuondoa vikwazo hivyo," alisema.

Alisema idadi hiyo ya vifo vya kina mama inachangiwa na kifafa cha mimba kwa asilimia 34, kupoteza dawa wakati wa kujifungua asilimia 24.7 na athari wakati wa uzazi asilimia 16.7 hivyo kwa ujumla asilimia 74 ya vifo vya kina mama wajawazito vinachangiwa na hali hiyo.

Dk.Bujari alisema utafiti umeonesha kuwa iwapo dawa muhimu zitafika kwenye hospitali na vituo vya afya kwa wakati upo uwezekano wa kuokoa wakina mama 11,113 kwa mwaka.

Aidha, Dk.Bujari alisema utafiti huo umeonesha kuwa iwapo dawa za kuongeza uchungu zitapatikana  kwenye vituo vya afya itasaidia kupunguza vifo 3,694 vya mama wajawazito nchini.

Alisema uwezekano wa kutokuwepo vifo vya kina mama ambao wamefikia umri wa kujifungua ni mkubwa iwapo changamoto hiyo ya kuchelewa kutoa dawa na zingine itatatuliwa.

Mkurugenzi huyo aliongezea kuwa utoaji dawa kwa wakati bandarini na MSD utaipungizia serikali gharama ya kulipia uhifadhi lakini pia itaokoa maisha ya wananchi wengi.

Aidha, alisema tatizo la vifo vya kina mama lipo vijijini zaidi hivyo nguvu kubwa ya uwepo wa huduma za msingi unahitajika.

No comments:

Post a Comment

Pages