Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akisaini mkataba
wa kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia na kuwa mojawapo
ya nchi kumi na mbili zilizosaini na kuridhia mkataba huo na
kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 60 zilizosaini na ya 32 zilizoridhia
mkataba huo. Zoezi hilo limefanyika katika jengo la Umoja wa Mataifa
kunakofanyika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa,New York, Marekani.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi akiwa katika picha ya
pamoja na mawaziri wa nchi 12 ambao wamesaini na wengine kuridhia mkataba wa
kupiga marufuku matumizi ya silaha za nyuklia na kuwa mojawapo ya nchi
kumi na mbili zilizosaini na kuridhia mkataba huo na kuifanya Tanzania kuwa
miongoni mwa nchi 60 zilizosaini na ya 32 kati ya zilizoridhia mkataba huo.
Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi
akisalimiana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ofisi
za Umoja wa Mataifa zilizopo New York, Marekani. Mazungumzo ya viongozi hao
yalilenga masuala ya maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki sambamba na
hali ya Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Na Mwandishi Wetu, New York
Umoja
wa Mataifa umeipongeza Serikali ya Jamhri ya Muungano wa Tanzania kwa mchango
wake wa kulinda amani katika ukanda wa maziwa makuu na kuahidi kushirikiana na
Tanzania katika kuzuia matukio yanayosababishwa na misimamo mikali.
Pongezi
hizo zimetolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alipokutana
na kufanya mazungumzo na Waziri wa Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Plamagamba John Kabudi ambapo pia katika mazungumzo hayo wamegusia masuala ya maendeleo
katika ukanda wa maziwa makuu, ikiwa ni pamoja na hali ya kisiasa ya Burundi na
usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Katibu
Mkuu Antonio Guterres amesema umoja huo unatambua mchango na jitihada za
Tanzania na kuongeza kuwa Umoja huo upo tayari kushirikiana na Tanzania katika jitihada
zake za kuzuia matukio yanayosababishwa na misimamo mikali.
Kwa
upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof.
Palamagamba John Kabudi ameuhakikishia Umoja wa Mataiafa kuwa Tanzania
itaendelea kushirikiana na Umoja huo
katika vikosi vya kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo
na sehemu nyingine duniani ili kuufanya ukanda wa maziwa makuu, Afrika na
duniani kwa ujumla kuwa mahali salama pa kuishi.
Ameongeza
kuwa Tanzania inaunga mkono mabadiliko yanayofanyika ndani ya Umoja wa Mataifa
na kwamba inakubaliana na mabadiliko hayo. Aidha, Waziri Kabudi ameitumia fursa
hiyo kumueleza katibu mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa hatua mbalimbali za
kimaendeleo ambazo Tanzania inatekeleza katika kufikia malengo ya maendeleo ya
Umoja wa Mataifa.
Katika
tukio jingine Tanzania imesaini mkataba wa kupiga marufuku matumizi ya silaha
za nyuklia na kuwa mojawapo ya Nchi kumi na mbili zilizosaini na kuridhia
Mkataba huo na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi 60 zilizosaini na ya 32
kati ya nchi zilizoridhia mkataba huo.
Prof.
Kabudi amesema kuwa Tanzania inaunga mkono jitihada zote za kupiga kabisa
marufuku matumizi ya silaha za nyuklia kama sehemu ya kuufanya ulimwengu kuwa
salama ambapo chini ya mkataba huu zimefanywa kuwa silaha za maangamizi.
Hata
hivyo Prof. Kabudi amesema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania haikatai na inaunga
mkono matumizi ya amani ya nguvu za nyuklia kama sehemu ya dawa, kuhifadhi
vyakula na uzalishaji wa nishati miongoni mwa matumizi mengine chini ya
uangalizi madhubuti wa shirika la kimataifa la nguvu za atomiki.
Ameongeza
kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua hiyo ikitiliwa maanani
kuwa zipo nchi zenye silaha za nyuklia takribani 14 elfu na zimetenga bajeti
kubwa kwa ajili ya kuimarisha silaha hizo na kutoa wito kwa mataifa hayo
kujenga imani kwa mataifa mengine na kwamba matumizi ya silaha hizo si njia
sahihi na salama za kuihakikishia dunia amani na usalama.
Prof.
Kabudi anatarajiwa kuhutubia katika mkutano wa 74 wa Baraza Kuu la Umoja wa
Mataifa baadae hii leo jijini New York, Marekani.
No comments:
Post a Comment