HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 05, 2019

TASAF yavifikia vijiji 40 Singida

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini, Rashid Mandoa akizungumza na baadhi ya waandishi wa habari na maofisa wa TASAF waliomtembelea ofisini kwake Septemba 4, 2019.



NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

VIJIJI 40 kati ya 84 vya Wilaya ya Singida Vijijini mkoani Singida vyenye kaya 7,760 vimenufaika na Mpango wa Kunusuru kaya maskini zaidi (TASAF).

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Vijijini, Rashid Mandoa alipozungumza na baadhi ya watendaji wa TASAF waliokwenda kufanya tathimini ya mpango huo.

Mandoa alisema tangu kuanza kwa mpango wa Kunusuru kaya maskini wilayani humo mwaka 2014 wanavijiji wengi wamejikwamua kwa kuongeza  vipato vyao.

"Hiki mnachokifanya ni kutoa mbegu kwa wahitaji ambao jukumu lao ni kuhakikisha mbegu hiyo inatoa mazao bora na endelevu.

"Kazi kubwa sana inafanywa na TASAF nawapongeza kwanza mnawekeza kwenye rasilimaliwatu hasa eneo la afya na elimu hili ni jambo la mfano kwa jamii yenye kiu ya maendeleo.

"Naamini kupitia ruzuku ya afya, watoto wengi hivi sasa wanapelekwa kliniki na idadi ya wanafunzi hasa wa kike pia imeongezeka shuleni maana wanapata ruzuku ya wasichana rika inayowasaidia kununua taulo za kike," alisisitiza Mandoa.

Alisema shuhuda za wanufaika wa mpango huo zinatia hamasa  na kuonesha namna inavyowezekana kwa mtu wa kipato cha chini kabisa kuwezeshwa na kuchangia pato la taifa.

Alisema walengwa wa TASAF wanafanya shughuli za kimaendeleo kwenye jamii zao ikiwemo kuchimba malambo ya maji, kujenga mifereji ili kuziia mafuriko wakati wa mvua, kujenga zahanati na kujiunga kwenyr vikundi vya kuweka na kukopa.

Akizingumzia lengo la ziara hiyo ya kutathimini shughuli zinazofanywa na walengwa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TASAF, Zuhura Mdungi, alisema ili kubaini changamoto za utekelezaji wa mpango huo na kutafuta mbinu sahihi za kukabiliana nazo.

"Mfano hapa wilayani wapo watoto wengi lakini tuliobahatika kuwafikia ni 4,092 tunahakikisha wanapelekwa kliniki na kupata huduma nyingine za afya panapohitajika na kubwa zaidi wanahudhuria masomo yao bila vikwazo," alisisitiza Tindikali.

No comments:

Post a Comment

Pages