HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 02, 2019

HAPATOSHI ATLAS SCHOOLS MARATHON 2019

>>Washiriki zaidi ya 2000 kuchuana, Bella, Beca Ibrozama kunogesha.
Mkurugenzi wa Shule za Atlas, Sylivanus Rugambwa, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusiana na mbio za Atlas Schools Marathon zitakazofanyika Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu Mkuu wa shule hizo, Joseph Mjingo. (Na Mpiga Picha Wetu).


NA MWANDISHI WETU

SHULE za Atlas Ubungo na Madale jijini Dar es Salaam, mwaka huu zinatarajiwa kuadhamisha mahafali na siku ya wazazi kwa aina yake ikiwamo mbio za Marathon.
Tukio hilo litafanyika Siku ya Kumbukumbu ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, Oktoba 14 kwenye kampasi ya Madale.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Makamu Mkuu wa shule, Joseph Mjingo, alisema; “Tofauti na miaka ya nyuma ambapom kulikuwa na sherehe za mahafali na siku ya wazazi pekee, kwa mara ya kwanza kutakuwa na mbio za barabarani zenye lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya ujenzi wa maktaba kubwa na ya kisasa ya umma ‘Public Library’ itajengwa katika kampasi ya Madale iliyopo Mivumoni Wilaya ya Kinondoni,”.

Mjingo, alisema mbio hizo zijulikanazo kama ‘Atlas Schools Marathon’ kutakuwa na Kilomita 5, 10 na Kilomita 21 ‘Nusu Marathon’, ambazo zitajumuisha wakimbiaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wa kulipwa na wa hiyari.

Makamu huyo mkuu wa shule, alisema mbio hizo zina baraka kutoka Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na kwamba ada ya ushiriki ni Sh. 25,000 kwa mbio zote, ambapo mshiriki atajipatia fulana, namba ya kukimbilia pamoja na medali baada ya kumaliza mbio.

Alizitaja zawadi kwa washindi wa Kilomita 21 Wanaume na Wanawake kuwa ni Sh. Milioni 1 kwa mshindi wa kwanza, wa pili Sh. 750,000, wa tatu 500,000, wa nne 300,000 huku wa tano akijipoza kwa Sh. 200,000.

Kwa upande wa Kilomita 10, mshindi atazawadiwa Sh. 500,000 wa pili 350,000, wa tatu 250,000, wan ne 150,000 na wa tano atajipoza kwa Sh. 100,000.

Mgeni rasmi katika mbio hizo zinazobeba kauli mbiu ya ‘Kimbia Kizalendo’, anatarajiwa kuwa Mbunge wa Karagwe, ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shule hizo, Sylivanus Rugambwa, alitoa wito washiriki kuchangamkia kujisajili kwa mbio hizo ili kufanikisha malengo hayo ya uchangiaji ujenzi wa maktaba.

Pia, alisema nafasi ziko kwa wadau mbalimbali kufanya biashara na kutoa huduma siku hiyo, ambako zaidi ya watu 2,000 watashiriki huku Christian Bella ‘Obama’ na Beca Ibrozama wakitumbuiza.

No comments:

Post a Comment

Pages