*Wapitisha miradi yote
mitatu iliyozinduliwa
Na Mwandishi Wetu
MWENGE wa Uhuru
uliokuwa unakimbizwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi umemaliza mbio zake na
kukabidhiwa wilayani Nachingwea.
Kiongozi wa
mbio za mwenge kitaifa, Bw. Mzee Ali Mkongea amesema miradi mitatu ya maendeleo
iliyopangwa kuzinduliwa wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.
Miradi hiyo
ni mabweni mawili kwenye shule ye sekondari ya wasishana ya Hawa Mchopa, mradi
wa maji wa Kitandi katika kata ya Likunja na mradi wa barabara ya lami kwenye
kata ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.
Akizungumza
na wananchi waliojitokeza kupokea mwenge huo leo asubuhi (Alhamisi, Oktoba 10,
2019) kwenye viwanja vya shule ya msingi Chiola, wilayani Nachingwea, Bw. Mkongea
amewataka wananchi wa wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye
uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi
huo, Novemba 24, mwaka huu.
Mapema, akizungumza na wakazi waliojitokeza kuupokea
mwenge huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwenge wa uhuru unakimbizwa
maeneo mbalimbali nchini ili kuwahamasisha wananchi washiriki kwenye shughuli
za maendeleo.
“Mwenge wa
Uhuru unakimbizwa kwenye maeneo yetu mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze
kushiriki kwenye miradi ya kujiletea maendeleo. Pia unaendana na kumbukumbu ya
kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hivyo,
tunakumbushwa kuyaenzi mawazo yake,” alisema.
Mbali ya
kuwahimiza washiriki kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri
Mkuu alisema kuna makundi manne ambayo yanapaswa kushiriki uboreshaji wa
taarifa zao kwenye Daftari la Mpiga Kura pindi zoezi hilo likianza.
“Wanaotakiwa
kushiriki zoezi hili, ni wale waliopoteza vitambulisho vyao au wanavyo lakini
vimefutika; waliohama maeneo yao na wako kwenye maeneo mapya ambako watapigia
kura mwakani; waliokuwa na umri chini ya miaka 18 mwaka 2015 na sasa wamezidi
umri huo; na wale ambao mwakani wanatarajia kufikisha umri wa miaka 18,” alisema.
Mapema, akizungumza baada ya kupokea mwenge
huo saa 2:45 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Bi. Rukia Muwango alisema leo
utakimbizwa kwenye wilaya hiyo ambapo miradi yenye thamani ya sh. milioni 781.5
itazinduliwa.
Kesho (Ijumaa,
Oktoba 11) mwenge huo utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na
Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na
kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment