HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 02, 2019

OFISA USALAMA SHIRIKA LA POSTA AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA KUSAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA

Ofisa Usalama wa Shirika la Posta Tanzania, George Mwamgabe (kushoto) na Abrahamani Msimu wakitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam wakikabiliwa mashtaka mawili likiwemo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin. (Picha na Francis Dande).  

Na Mwandishi Wetu

WATU wawili akiwemo Ofisa Usalama wa Shirika la Posta Tanzania, George Mwamgabe (44) wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa mashtaka mawili ikiwamo la kusafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin. 
Mbali na Mwamgabe, mshtakiwa mwingine aliyefikishwa mahakamani hapo ni  Abrahamani Msimu (54) dereva na mkazi wa Yombo jijini Dar es Salaam. 

Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustina Mmbando na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali Aldolf Lema. 

Lema alidai kuwa  Agosti 25 mwaka jana katika eneo la Posta jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao kwa pamoja walisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 124.55.

Katika shtaka la pili, Wakili Lema alidai Agosti 25, 2018 katika eneo la Posta washtakiwa wote kwa pamoja walisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin yenye uzito wa gramu 1.55.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo washtakiwa wote walikana kutenda makosa yao, upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika. 

Hakimu Mmbando akitoa masharti ya dhamana aliwataka kila mshtakiwa kuwa na wadhamini wawili mmoja kutoka ofisi za umma watakaosaini bondi ya Sh. Milioni tano kila mmoja. 

Hata hivyo washtakiwa hao wameshindwa kutimiza masharti ya dhamana hivyo wamerudishwa rumande hadi Oktoba 16 mwaka huu kesi hiyo itakapokuja tena kwa ajili ya kutajwa.

No comments:

Post a Comment

Pages