Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimshukuru Katibu wa CWT Mkoa wa Songwe
Bi Emilia Mwakyoma kwa niaba ya CWT Taifa kwa mchango wa mifuko 400 ya saruji
itakayosaidia katika kuboresha miundombinu ya madarasa Mkoa wa Songwe. Katikati
ni Afisa Elimu Mkoa wa Songwe Juma Kaponda.
Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John
Palingo (kulia), kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mkoa wa Songwe mchango
wa Chama cha Waalimu Nchini (CWT) mifuko 400 ya saruji kwa ajili ya kuboresha
miundombinu ya elimu Mkoani Songwe.
Na Mwandishi Wetu, Songwe
Chama cha Waalimu
Tanzania (CWT) kimeunga Mkono maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ya ukamilishaji wa maboma ya Vyumba vya
madarasa, kwa kuchangia Mifuko 400 ya saruji Mkoa wa Songwe.
Katika ziara yake
Mkoa wa Songwe Rais Magufuli alipokea taarifa ya bakaa ya shilingi billioni
Mbili ambapo alielekeza fedha hizo zitumike kukamilisha mabomba ya shule ambayo
yamejengwa kwa nguvu za wananchi hususani katika Wilaya ya Mbozi.
Akikabidhi mchango huo
kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CWT, Katibu wa CWT Mkoa wa Songwe Bi Emilia
Mwakyoma amesema Chama cha Waalimu kinapongeza Serikali kwa kuhimiza uboreshaji
wa miundombinu ya Elimu.
“Tunapongeza sana
Juhudi za Serikali ya awamu ya tano na sisi kama wadau wa elimu tumechangia na
tutaendelea kuchangia kwakuwa tunatambua kuwa serikali inatengeneza miundombinu
mizuri ya wanafunzi kujifunzia pia waalimu watakuwa na mazingira mazuri ya
kufanyia kazi.”, amesema Mwakyoma.
Mkuu wa Mkoa wa
Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameipongeza CWT kwakuwa licha ya kutetea
haki za waalimu wamekuwa mstari wa mbele katika kuthamini na kuchangia miundombinu
ya elimu hasa kwa Mkoa wa Songwe.
Brig. Jen. Mwangela
amesema mchango huo unapelekwa maeneo yenye uhitaji Zaidi huku akieleza kuwa
Wilaya ya Mbozi mpaka sasa ina maboma 1510 hivyo wadau wengine wajitokeze kuendelea
kuboresha miundombinu ya elimu Mkoani Songwe.
Naye Afisa Elimu Mkoa
wa Songwe Juma Kaponda amesema kwa Mkoa wa Songwe jumla ya maboma 1601
yanaendelea kujengwa huku halmashauri ya Mbozi ikiongoza kwa kuwa na maboma
mengi yaani 1510.
Naye Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Msanyila Wilayani Mbozi Gwakisa Mwalusaku amesema shule hiyo
imejenga vyumba 16 ambapo mifuko kumi ya saruji waliyopokea kutoka CWT
itaharakisha ukamilishaji wa vyumba hivyo.
No comments:
Post a Comment