Na Tatu Mohamed
JAMII imetakiwa kutokuvifumbia macho vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto kwani ni kinyume na haki za binadamu.
Wito
huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Kamishna wa Tume ya Haki za
Binadamu, Nyanda Shughuli katika maadhimisho ya Siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia yaliyoandaliwa na TGNP mtandao yenye kauli mbiu ya
'Kizazi cha Usawa, Simama dhidi ya Ubakaji'.
Alisema
ni vyema suala la ukatili wa kijinsia likatazamwa kwa jicho la tofauti,
kwani bado kuna kazi kubwa katika jamii ya kubadili mtazamo pamoja na
fikra.
"Nitoe wito kwa
jamii isivifumbie macho vitendo hivi, vinaumiza sana na ni kinyume na
haki za binadamu. Mnapokutana na matukio mbalimbali ya aina hii
mshirikiane na vyombo husika, hii itawezesha kuwachukulia hatua
wanaoendeleza vitendo hivi," alisema Shuli.
Aliongeza kuwa tume itaendelea kuelimisha jamii ili kuhakikisha wanawake na haki za watoto zinazingatiwa.
"Taifa
lisilo na ukatili wa kijinsia ni taifa lenye maendeleo ya kasi.
Tulitazame suala hili kwa jicho la tofauti. Tuendelee kushikamana
kuhakikisha kila mmoja katika nafasi yake anapambana kuvitokomeza,"
alisema Nyanda.
Naye
Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP Mtandao, Lilian Liundi, alisema ukatili dhidi
ya wanawake unaathari kubwa si tu kwa wanawake bali pia katika uchumi
wa nchi na maendeleo pamoja na ustawi wa jamii kwa ujumla.
"Tanzania
ya Viwanda Wanawake ni Msingi wa mabadiliko ya kiuchumi.
Tunpozungumzia Tanzania ya viwanda wakati wanawake zaidi ya asilimia 30
wanaendelea kufanyiwa ukatili wa kijinsia hivyo hawawezi kushiriki
kikamilifu katika maendeleo ya nchi ni changamoto kubwa sana.
"Mimi
naamini kuwa kukiwa na mgawanyo mzuri wenye usawa, wanawake na
wasichana wataweza kufikia fursa za kiuchumi na maarifa itawasaidia
kufanya maamuzi mazuri katika familia na jamii na kuongeza kasi ya
maendeleo," alisema.
Aidha
alisema tunapoelekea kuadhimisha miaka 25 ya Ulingo wa Beijing, pia
tunapaswa kutafakari kwa kina hatua iliyopigwa katika kutokomeza vitendo
vya ukatili wa kijinsia na kuweka mikakati itakayowezesha kukomesha
kabisa ili kuweza kufikia maendeleo endelevu.
No comments:
Post a Comment