Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi akiangalia moja ya Majalada katika ofisi ya Ardhi ya Halmashauri
ya Wilaya ya Mvomero.
Na Munir Shemweta,
WANMM MVOMERO
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli amebatilisha pendekezo la kufutwa shamba lenye ukubwa wa ekari 1000 lililopo
Kidunda wilayani Mvomero mkoani Morogoro linalomilikiwa na Cecilia George
Rusimbi.
Uamuzi wa Dkt Mafuli kubatilisha ufutaji shamba hilo
unatokana na kubainika kuwa pendekezo lililowasilishwa la kufutwa shamba hilo
kwa madai ya kutoendelezwa kutokuwa za kweli na ulilenga kumdhulumu mmiliki
wake.
Akitangaza uamuzi huo wa Raisi jana wilayani Mvomero, Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema, baada ya
kufuatilia mashamba yaliyopendekezwa kufutwa Dkt Magufuli alibaini taarifa alizopelekewa
za kufuta shamba Cecilia hazikuwa sahihi na hivyo kuamua kubatilisha pendekezo
lililowasilishwa kwake na kumpatia haki yake mmiliki.
Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi aliwaonya Aaafisa ardhi
nchini kuhakikisha wakati wa kufanya zoezi la ukaguzi/Upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa
wanazingatia haki pamoja na kufuata sheria badala ya kufanya kazi hiyo kwa
upendeleo au kumuonea mtu.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alisema, utendaji kazi katika
wilaya ya Mvomero umekuwa wa hovyo na usiozingatia maadili jambo linalopelekea wilaya
hiyo kuongoza katika mkoa wa Morogoro kuwa na migogoro mingi ya ardhi sambamba
na malalamiko mengi ya wananchi dhidi ya ofisi ya ardhi.
‘’Baadhi ya watumishi katika ofisi ya halmashauri ya wilaya
ya Mvomero mnajifanya ni Maafisa ardhi au Wapima wakati hamkuajiriwa kwa nafasi
hiyo, mnasaini nyaraka za ardhi na kuwaumiza wananchi’’ alisema Lukuvi
Kwa upande wake Cecilia George Rusimbi alimshukuru Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa uamuzi wake wa
kubatilisha ufutaji sahamba lake na kuuelezea uamuzi huo kuwa umezingatia haki na kusikia kilio chake ambapo
alisema umempa faraja baada ya kuhangaika sana kuhusiana na shamba hilo.
‘’ Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987 na kuhangaikia hati kwa
muda mrefu na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba langu liko katika mpango wa
kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii imenifanya kuishi kwa wasiwasi’’ alisema
Cecilia.
Waziri Lukuvi ameagiza shamba hilo la kilimo cha Michikichi,
Mitiki na Bamboo kupangwa upya na mmiliki
wake kupatiwa hati kulingana na upimaji utakaofanywa na kumtaka kuliendeleza
kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na sakata la shamba la Cecilia, Lukuvi aliagiza
kupunguzwa ukubwa wa Shamba Sangasanga na Lubango lililodaiwa kuwa na ukubwa wa
ekari 1,103 wakati uhalisia wa shamba hilo ni ekari 500 na kuagiza mmiliki wake
kurudisha hati ili apatiwe hati ilinayolingana na uhalisia wake na ekari 603.5 zilizoongezwa
zitabaki kuwa ardhi ya akiba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl Mohamed Utaly alieleza
kuwa wilaya yake ina tatizo kubwa la migogoro ya ardhi pamoja na jitihada kubwa
inayofanywa na ofisi yake kukabiliana na tatizo hilo na kuongeza kuwa mingine
inachochewa na uhamasishaji unaowafanya wananchi kukata tamaa.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi William Lukuvi alitembelea ofisi ya Ardhi katika halmashauri ya
Mvomero na kubaini ‘madudu’ katika ofisi hiyo ambapo alibaini baadhi ya majalada
ya wananchi waliomba kumilikishwa ardhi tangu mwaka 2012 katika halmashauri
hiyo kushindwa kupatiwa hati huku.
Hali hiyo ilimfanya Waziri Lukuvi kumuagiza Kaimu Kamishana Msaidizi
wa Ardhi Kanda Maalum ya Morogoro Erick Makundi kuhakikisha wale wote walioomba hati
na kutumiza vigezo vya kupatiwa hati wanapatiwa kufikia mwezi ujao Desemba
2019. Pia ameagiza kufuatiliwa majalada 300 ambayo wamiliki wake wamekamilisha
taratibu za kupatiwa hati lakini hawajapatiwa.
Sambamba na hilo Lukuvi aliagiza wafanyakazi wa ofisi ya
ardhi katika halmashauri hiyo wanaojitolea kutosaini nyaraka zozote za ardhi
kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishiriki kutoza tozo kwa gharama
za juu za shilingi 50,000 wakati gharama halisi ni 20,000.
No comments:
Post a Comment