Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula, akimsikiliza
Mkuu wa Wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro Mathayo Masele wakati akikagua maendeleo
ya ujenzi wa jengo la Halmashauri ya wilaya ya Malinyi unaofanywa na Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya
ardhi mkoani Morogoro mwishoni mwa wiki. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir Shemweta, WANMM ULANGA
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angelina Mabula amemtaka Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro kumpatia maelezo kuhusiana na
uamuzi wake wa kuondoa kasma ya ardhi na mipango miji kwenye bajeti ya mapato
ya ndani baada ya sekta hiyo kuhamishiwa Wizarani.
Uamuzi huo wa Dkt Mabula
unafuatia kuelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ulanga Ngollo Malenya kuwa moja ya
changamoto inayoikabili sekta ya ardhi kwenye wilaya yake ni ukosefu wa fedha
za uendeshaji wa ofisi uliosababishwa na halmashauri kuondoa kasma ya ardhi na
mipangomiji baada ya sekta hiyo kuhamia wizara ya ardhi jambo alilolieleza
limesababisha utekelezaji majukumu ya kila siku kuwa magumu.
Akiwa katika ziara yake
ya siku moja katika wilaya hiyo mwishoni mwa wiki, Naibu Waziri huyo wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimtaka Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
wilaya ya Ulanga Juma Kapilima kumpa taarifa ya maandishi kuhusiana na suala
hilo kwa kuwa Waraka uliotolewa kuhusiana na suala hilo unaeleza wazi kilichohamishiwa
wizarani ni Mamlaka ya Nidhamu na Ajira pekee.
‘’Hii ni serikali moja,
ofisi ya Mkurugenzi ni Mamlaka ya upangaji, nataka maelezo ya msingi maana waraka unajieleza na ulienda
kwa Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya na hata mishahara ya watumishi wa sekta
ya ardhi bado inalipwa na TAMISEMI’’ alisema Dkt Mabula,
Kwa mujibu wa Mkuu wa
wilaya ya Ulanga, mbali na changamoto ya ukosefu wa fedha katika sekta ya ardhi,
wilaya yake inakabiliwa pia na uchache wa watumishi hususan katika fani za
Mipango Miji, Uthamini, Uchoraji Ramani na Watunza Kumbukumbu alioueleza kuwa
unasababisha shughuli zilizopangwa kutofanyika kwa ufanisi.
Aidha. Naibu Waziri Mabula
alionesha kutoridhishwa na kasi ya zoezi la urasimishaji na upimaji viwanja kwenye
wilaya ya Ulanga na kueleza kuwa halmashauri hiyo inatakiwa kuongeza kasi
katika mazoezi hayo mawili ili kuwa na mji uliopangika na kuepuka ujenzi
holela.
Aliongeza kwa kusema,
katika zoezi la urasimishaji linaloendelea nchini halmashauri ya Ulanga inatakiwa kukaa na
wananchi pamoja na makapuni ya urasimishaji ili kukubaliana gharama za
urasimishaji na kusisitiza kiwango cha shilingi 150,000 kilichowekwa na Wizara
kinaweza kupungua ili kuwafanya wananchi wengi kushiriki,
‘’Kuna halmashauri
zimekubaliana na makampuni ya urasimishaji ambapo gharama zimepungua hadi kufikia
60,000 hivyo ninyi hapa msing’ang’anie kiwango cha 150,000 maana kinaweza
kupungua kulingana na ugumu wa kazi na idadi ya watu waliojitokeza
kurasimishwa’’. Alisema Dkt Mabula
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Dkt Angeline Mabula ametembelea wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro na
kuitaka wilaya hiyo kuongeza kasi ya upimaji, upangaji na umilikishaji ardhi na
kuzingatia kupanga mji wa kiserikali utakaojumuisha taasisi zote za umma.
Aidha, Dkt Mabula
alikagua ujenzi wa jengo la halmashauri ya wilaya ya Malinyi pamoja na nyumba
ya Mkuu wa wilaya unaofanywa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambapo alionesha kufurahishwa na kasi ya
ujenzi wa majengo hayo mawili yanayotarajiwa kukabidhiwa rasmi mwanzoni mwa mwaka ujao 2020.
No comments:
Post a Comment