Na Benny Mwaipaja, Dar es
Salaam
Rais na Mtendaji Mkuu wa
Benki ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt.
Admassu Tadesse ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kutekeleza mradi mkubwa wa
ujenzi wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (SGR) kwa kutumia fedha zake za ndani na
kuahidi kuwa Benki yake itafanya kila linalowezekana kuhakikisha inatafuta
fedha za kujenga reli hiyo
Dkt.
Tadesse ametoa kauli
hiyo alipotembelea sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya reli hiyo, kipande
cha Dar es Salaam hadi Morogoro na kujionea kazi kubwa iliyofanyika
ambapo
amesema mradi huo hautainufaisha Tanzania peke yake bali pia nchi za
ukanda wa
Afrika hususan ambazo hazipakani na Bahari.
Kiongozi huyo wa juu wa Benki
ya Biashara na Maendeleo Mashariki na Kusini mwa Afrika (TDB) Dkt. Tadesse,
ameeleza kuwa mwaka huu Benki yake imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti
nafuu wa dola za Marekani bilioni moja sawa na takribani sh. za Tanzania
trilioni 2.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi yake mikubwa ya maendeleo.
Ameongeza
kuwa Tanzania
imenufaika pia na kiasi kingine cha zaidi ya dola za Marekani bilioni
moja zilizotolewa na Benki yake miaka ya nyuma na ameelezea kufurahishwa
kwake na namna
nchi inavyokua kwa kasi kiuchumi na kwamba inakopesheka.
Aliahidi kuwa kwa kuwa fedha
zinazohitajika kukamilisha ujenzi wa mradi huo wa reli ya kisasa ni nyingi,
Benki yake itazishawishi taasisi nyingine za fedha ndani na nje ya Bara la
Afrika kuchangia ujenzi huo ili mradi ukamilike kwa wakati ili kuchochea
masuala ya Bashara na kuboresha shughuli za usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo.
Kwa upande wake Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) Bw. Masanja Kadogosa, ameishukuru Benki hiyo
kwa kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa Reli hiyo katika awamu zinazofuata.
Alisema kuwa mpaka sasa
ujenzi wa Reli ya Kisasa ambao umetumia fedha za ndani kati ya Dar es Salaam
hadi Morogoro umekamilika kwa asilimia 72 huku kipande cha Morogoro hadi Makutupora
mkoani Singida kikiwa kimekamilika kwa asilimia 22.
Bw. Kadogosa amesema kuwa
Serikali inatafuta fedha nyingine kwa ajili ya kujenga reli hiyo kuanzia Makutupora, Tabora, Isaka hadi Mwanza
na kwamba watafanya mazungumzo na Benki hiyo kuona namna watakavyofadhili
ujenzi huo.
No comments:
Post a Comment