Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, William Lukuvi, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Magomeni Wilaya
ya Kilosa mkoani Morogoro (hawapo pichani), alipokwenda kusikiliza
malalamiko ya wakazi hao kuhusiana na shamba la Mwekezaji Farm
Africa Agro Focus Ltd. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi. (Picha na Wizara ya Ardhi)
Na Munir Shemweta,
WANMM KILOSA
Wananchi wa Kijiji cha Magomeni kilichopo tarafa ya Kilosa
Mjini wilayani Kilosa mkoani Morogoro wametoa kilio chao kwa Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakitaka kupatiwa shamba la
Mwekezaji Farm Africa Agro Focus Ltd marufu kama 'Kwa Karamagi,' kwa madai kuwa
mwekezaji wa shamba hilo ameshindwa kuliendeleza.
Wananchi hao wamemueleza Lukuvi kuwa, kijiji hicho hakina
ardhi ya kutosha kuwawezesha kujishughulisha na kilimo na kwamba eneo
kubwa katika kijiji hicho ni la shamba la Farm lenye ukubwa wa ekari
13,000.
Wananchi hao walitoa kilio chao kwa
Waziri Lukuvi, Novemba 8, 2019, wakati waziri huyo akiwa katika ziara yake
wilayani Kilosa kuendelea na jitihada za kutatua migogoro ya ardhi katika mkoa
wa Morogoro.
Wamedai kuwa pamoja na mwekezaji kuwa na eneo kubwa, lakini
ameshindwa kuliendeleza kama taratibu zinavyotakiwa na badala yake sehemu kubwa
ya shamba hilo imebaki kuwa pori ingawa limeendelezwa katika eneo la usoni.
Mmoja wa wananchi hao Ismail Masudi alimueleza Waziri Lukuvi kuwa wananchi wa kijiji hicho wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa kutokana na mgogoro wa muda mrefu
kati ya mwekezaji na wananchi hao.
‘’Wananchi tumepiga kelele sana ya kusaidiwa, Mwekezaji ana
eneo kubwa, lakini wananchi wanakosa maeneo ya makazi na ya kufanyia shughuli za
kilimo, huku sehemu kubwa ya shamba la mwekezaji ikiwa ni pori,’’ alisema Masudi
Mwananchi mwingine Hatibu Musa alisema kilio kikubwa cha
wakazi wa kijiji hicho ni eneo la kulima, wakati idadi ya wakazi
inaongezeka na wananchi wamehangaika kwa takriban miaka mitano na mgogoro huo, huku wakidai
mwekezaji hana tija.
Kwa upande wake Waziri Lukuvi alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi, kumuomba mwekezaji
wa shamba hilo kupunguza ekari 3000 kati ya 13,000 alizokuwa nazo kwa ajili ya kuwapatia
wananchi wa kijiji cha Magomeni.
"Badala ya kuanza kufuta shamba, Mwekezaji arudishe ekari
3000 kati ya 13,000 alizokuwa nazo tunataka kasi ya uendelezaji iendelee maana
haiwezekani miaka nane ni ekari 2000 tu zilizoendelezwa,’’ alisema Lukuvi.
Alisema, haingilii maamuzi ya mahakama yaliyompa ushindi
Mwekezaji na wala hataki wananchi kupingana na maamuzi ya mahakama, bali hali
hiyo inafuatia mwekezaji kushndwa
kuliendeleza shamba kama taratibu zinavyotakiwa ambapo uendelezwaji unatakiwa
kufanyika moja ya nane kila mwaka jambo alilolieleza mwekezaji huyo alishindwa
kutekeleza.
Taarifa kuhusiana na shamba hilo zinaeleza kuwa Mwekezaji wa
sasa Farm Africa Agro Focus alikabidhiwa shamba mwaka 2013 hadi kufikia sasa
ni ekari 2000 pekee kati ya 13,000 ndizo zilizoendelezwa kwa kulima zao la
Korosho.
No comments:
Post a Comment