Mwenyekiti wa (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu akiongea na wafanyakazi wa tume pamoja na wageni wengine waliohudhuria hafla fupi.
Na Mbaraka Kambona
Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu, ametembelea ofisi za taasisi hiyo zilizopo visiwani Zanzibar, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu alipokabidhiwa dhamana hiyo Novemba 4, 2019.
Jaji Mwaimu alifanya ziara hiyo mapema leo (Novemba 30, 2019) kwa lengo la kutambuana na wafanyakazi wa tume waliopo katika ofisi hizo zilizopo Mbweni, visiwani Zanzibar.
Katika ziara hiyo, Jaji Mwaimu akiongozana na Makamishna na viongozi wengine wa tume alifanya ukaguzi wa ofisi hizo ambazo hivi karibuni zilifanyiwa ukarabati mkubwa kwa lengo la kuziboresha.
Akizungumza baada ya kumaliza ukaguzi wa jengo hilo, Jaji Mwaimu alieleza kuridhishwa kwake na ukarabati huo uliofanyika, na kusema kuwa watajipanga vizuri katika majukumu yao ili kuhakikisha wanazitumia vizuri ofisi zote mbili za Tanzania bara na hizo za visiwani
ili kutatua kero za wananchi.
Aidha, Jaji Mwaimu aliwashukuru Shirika la Kimataifa la Maendeleo (UNDP) kwa ufadhili wao ambao umewezesha kufanikisha ukarabati huo.
Katika ziara hiyo Jaji Mwaimu aliambatana na viongozi wafuatao; Makamu Mwenyekiti, Mohamed Khamis Hamad, Mheshimiwa, Dkt. Fatma Rashid Khalfan, Mheshimiwa Thomas Masanja, Mheshimiwa Amina Talib Ali, Mheshimiwa Khatib Mwinyi Chande na Mheshimiwa Nyanda Josiah Shuli.
No comments:
Post a Comment