HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 01, 2019

JOWUTA wachagua viongozi wapya

 Mwandishi Mwandamizi wa Gazeti la TanzaniaDaima, Suleiman Msuya akichangia mada kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo Habari  Tanzania (JOWUTA), uliofanyika jijini Dodoma. (Picha na Kenneth Ngelesi).
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi katika vyombo vya habari Tanzania (JOWUTA), Cloud Gwandu, akizungumza katika mkutano wa kuchagua viongozi wapya wa chama hicho. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti, Ramadhan Libenanga na kulia ni Katibu, Suleiman Msuya.

 
Na Mwandishi Wetu, Dodoma

CHAMA cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania  (JOWUTA), kimepata viongozi wapya ambao watadumu kwa kipindi cha miaka mitatu.

Uchaguzi huo umefanyika katika ukumbi wa Maktaba ya Mkoa wa Dodoma jijini hapaambao wanachama 48 walishiriki kati ya 61 waliothibitisha kushiriki.

Mwenyekiti wa Uchaguzi huo Keneth Ngelesi alitangaza washindi katika uchaguzi huo ambapo nafasi ya Mwenyekiti mshindi ni Mwandishi Mkongwe Claud Gwandu aliyeibuka mshindi kwa kura 30 dhidi ya Sitta Tuma aliyepata kura 17.

Ngelesi alitangaza kuwa nafasi ya Makamu Mwenyekiti ilikuwa na mgombea mmoja Ramadhan Libenanga ambaye alipata kura 43 za ndio na nne hapana.

"Nafasi ya Katibu Mkuu wa JOWUTA mshindi ni Suleiman Msuya kwa kupata kura 44 za ndio tatu hapana na moja iliharibika na Said Mmanga amechaguliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu kwa kupata kura 46 za ndio na mbili za hapana," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema katika nafasi ya mweka hazina wajumbe walimpigia kura 47 za ndio Maurine Odunga kuendelea kushika nafasi hiyo huku kura moja ikiwa ya hapana.

Ngelesi alisema wajumbe waliwachagua Veronica Ignatus, Mussa Juma na Saphia Ngalapi kuwa wadhamaini wa chama.

Akizungumza baada ya uchaguzi Mwenyekiti mpya wa JOWUTA, Gwandu alisema mafanikio ya chama hicho yatatokana na wanahabari wenyewe kukijenga.

Gwandu aliwaomba waandishi wote nchini kutumia chombo hicho kupigania haki, maslahi  na maendeleo yao na nchi.

"Nawaomba wenzangu tushitikiane kuijenga JOWUTA na ili hilo lifanikiwe ni wajibu wa kila mmoja kutafuta wanachama kuanzia 10 wajiunge tuende pamoja kudai haki zetu kisheria," alisema.

Mwenyekiti hiyo aliwataka wanachama wajitahidi kulipa ada ya kila mwezi ili kuwezesha chama kujiendesha chenyewe na kufuatilia stahiki za waandishi kisheria.

Mbali na uchaguzi wa viongozi mkutano huo ulifanya mabadiliko ya kiingilio kutoka shilingi 5,000 na kuwa shilingi 10,000/.

JOWUTA ilisajiliwa mwezi Machi mwaka jana ambapo kwa sasa kina wanachama zaidi 120  katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tabora, Arusha, Mbeya na Mwanza.

Uchaguzi huo umefanyika baada ya Jowuta kuwa chini ya uongozi wa muda ambapo Said Mmanga alikuwa Mwenyekiti, Saphia Ngalapi, Makamu Mwenyekiti, Samson Kamalamo, Naibu Katibu Mkuu na Maureen Odunga, Mwekahazina.

Jowuta ilisajiliwa Machi, 2018 baada ya Mahakama Kuu, kitengo cha Kazi kukifuta kilichokuwa Chama cha Wafanyakazi Waandishi wa Habari Tanzania (TUJ), mwaka 2014, kufuatia maombi ya msajili wa vyama vya wafanyakazi na waajiri.

No comments:

Post a Comment

Pages