Mbunge wa jimbo la Busega, Mhe. Dkt. Rafael Chegeni akizungumza katika tamasha la Lamadi Utalii Festival linaloendealea katika shule ya Itongo, Lamadi,Busega Mkoani Simiyu.
Na Andrew Chale, Busega
MJI wa Lamadi uliopo katika Wilaya ya Busega Mkoa wa Simiyu hapa nchini unatarajiwa kujengwa kituo cha Maajabu kitakachokuwa kinatembelewa na watalii ulimwenguni kote 'Disney land'.
Akizungumza katika tamasha la kukuza na kuendeleza Utalii Wilaya ya Busega la 'LAMADI UTALII FESTIVAL ', linaloendelea mjini hapa, Mbunge wa jimbo la Busega Dkt. Rafael Chegeni amesema wanataka mji huo kuwa wa kitalii na wenye kuleta tija katika maendeleo ya kiuchumi kama miji mingine mikubwa Duniani.
"Sasa hivi tunategemea kupata mwekezaji ambaye atajenga kituo cha maajabu ya kidunia 'Disney land '.
Watu watakuwa wanafanya Utalii kutoka pande zote za dunia na Disneyland hii itajengwa hapahapa Busega maeneo ya Kijereshi na tayari mwekezaji yupo tayari 2020 kuanza ujenzi wa mradi huu.
Hii itasaidia sana kufungua fursa za kiuchumi kama Sera ya CCM inavyoeleza katika kumuinua mwananchi kiuchumi" alisema Dkt. Chegeni.
Aidha, Dkt. Chegeni ametoa wito kwa Wananchi wa Busega kuendeleza ujirani mwema na hifadhi huku pia akitaka kulindwa na kuendelezwa sehemu za kijadi ikiwemo Dom za machifu 'Chief Kingdom'.
"Utalii ni wetu wote na hata Serikali yetu ya Chama cha Mapinduzi imebainisha kwamba moja ya mapato muhimu kwenye serikali yetu, yanatokana na Utalii.
Na wizara ya Maliasili na Utalii inaongoza kwa kuchangia kwenye mfuko mkuu katika Gawio kwa Serikali kwani Gawio linalotolewa Serikalini sio la kawaida na tunawapongeza Mawaziri wa Wizara hii Constantine Kanyasu na Waziri Dkt. Hamisi Kigwangalla." alisema Dkt. Rafael Chegeni.
Dkt. Chegeni aliongeza kuwa, Wananchi wa Lamadi kiu yao ni kuona Utalii uliopo hapa iwe sehemu ya kukuza uchumi.
"Wananchi wa Lamadi kiu yetu ni kuona kwamba utalii uliopo hapa iwe sehemu ya kukuza uchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Busega na hata wilaya za jirani na Watanzania wote ndio maana tukasema kila mwaka tuwe na tamasha ili kwa maana ya kwamba tuchochee watu wathamini maana ya kuwa na utalii". Alieleza Dkt. Chegeni.
Aidha, Dkt. Chegeni aliongeza kuwa, sasa hivi Lamadi inatakiwa iwe kama miji mingine ya Kitalii kama Karatu ambapo watalii wengi wanalala Karatu na kutembelea Serengeti na Ngorongoro hivyo suala hilo liwe pia upande huo watalii kulala Lamadi na kutembelea Serengeti.
Katika hatua nyingine Dkt. Chegeni alisema wataangalia namna ya kuendeleza eneo mji wa Gambushi iliopo ndani ya mkoa wa Simiyu.
Tamasha lenye kauli mbiu "Utalii wa Ndani unawezekana" limedhaminiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na wadau wengine mbalimbali.
No comments:
Post a Comment