HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 31, 2019

TABORA WATAKIWA KUTATUA MIGOGORO YA ARDHI ILI KUWEKA MAZINGIRA MAZURI YA UWEKEZAJI

 Mtaalamu Mwelekezi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) Dkt. Hoseana Lunogelo akitoa maelezo mafupi leo kwenye kikao cha kupata maoni juu ya mwongozo wa uwekezaji  wa Mkoa wa Tabora.  (Picha na Tiganya Vincent).
 Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey akifungua kikao maalumu cha wadau cha kutoa maoni ya juu ya kuboresha mwongozo wa uwekezaji  wa Mkoa wa Tabora.
 Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Gift Msuya akitoa maoni yake jana  kwenye kikao cha kupata maoni ya juu ya mwongozo wa uwekezaji  wa Mkoa wa Tabora.
 Baadhi ya wadau wakiwa kwenye kikao cha kupata maoni ya juu ya mwongozo wa uwekezaji  wa Mkoa wa Tabora leo.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri( wa tatu kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Wataalamu kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) na Wakuu wa Wilaya, Wenyeviti wa Halmashauri za wilaya mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kupata maoni ya juu ya mwongozo wa uwekezaji  wa Mkoa wa Tabora.
 
 
Na Tiganya Vincent, Tabora

HALMASHAURI za wilaya Mkoani Tabora zimetakiwa  kuhakikisha zinamaliza migogoro ya ardhi iliyopo kwa ajili kuweka mazingira ambayo yatawavutia wawekezaji ili waweze kutumia fursa zilizomo kwa ajili ya kuwekeza kwenye miradi ya maendeleo kwa manufaa ya Mkoa na wakazi wake.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mtaalamu Mwelekezi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) Dkt. Hoseana Lunogelo kwenye kikao cha kupata maoni ya juu ya mwongozo wa uwekezaji  wa Mkoa wa Tabora.

Alisema kuwa Mkoa wa Tabora unayo maeneo mengi ambayo yanafaa kwa uwekezaji lakini uwekezaji unaweza kukwama pindi panapo kuwepo na eneo ambalo linaonekana lina mgogoro miongoni mwa jamii na Halmashauri husika.

Dkt. Lunogelo alisema kuwa Tabora ni moja ya Mikoa hapa nchini ambayo imekaa vizuri kutokana na Jiografia yake na miundombinu yake inaunganisha na mikoa inayoizunguka hivyo kuwa na uwezo wa kusafirisha  bidhaa zinazozalishwa  na kufika sokoni kwa urahisi.

Aliongeza kuwa Mkoa huo  unayo fursa kubwa kwa uwekezaji zao la asali kwani wilaya zake zimezungukwa na misitu ya miombo ambayo ni malisho mazuri ya nyuki ambayo inaweza kusaidia katika ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha kusindika asali kwa sababu ya uhakika wa kupata malighafi.

Kwa upande wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Msalika Makungu alizitaka Halmashauri za Wilaya kuhakikisha zinatenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na pale inapoonekana kuna vikwazo kutokana na wananchi kudai fidia dhidi ya  maeneo yao wawalipe mapema.

Alisema sio vizuri wawekezaji wapewe eneo ambalo lina migogoro hatua hiyo itasababisha waende maeneo mengine kwa ajili ya kutafuta maeneo ambayo wana uhakika wa uwekezaji wao.

Aidha Makungu aliwaomba Wenyeviti wa Halmashauri kutumia vikao vya Mabaraza ya Madiwani kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa na wananchi wanalijua ili wawekezaji wasikwamishwe na migogoro ya ardhi.

Alisema hatua hiyo itasaidia wawekezaji waweze kufika na kuwekeza katika maeneo yaliyo ndani ya Halmashauri zao  bila ya vikwazo na kusababisha kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Katika kikao hicho baadhi ya wachangiaji mbali mbali kutoka Halmashauri za wilaya hiyo walisema ni vema maeneo ya uwekezaji yakawa na miundombinu mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa maji, barabara, umeme na kuwa maeneo yenye hati ili kuwavutia wawekezaji.

Mkoa uliitisha Kikao cha wadau kwa ajili ya kupata maoni na ushauri ili kuthibitisha mwongozo wa andiko la fursa za uwekeazi  wa Mkoa wa Tabora.


Mkutano huo ni matokeo ya Jukwaa la Biashara na Uwekezaji lililofanyika Mkoani humo Novemba mwaka jana na kufunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa.
 

No comments:

Post a Comment

Pages