HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 17, 2020

Flora, Fauna kukutanisha wakulima Moshi

NA SULEIMAN MSUYA

SHIRIKA la Flora & Fauna Restoration System Tanzania limeandaa maonesho ya kubadilishana uzoefu, biashara, kujifunza mbinu bora za kilimo na kutanua wigo wa kilimo hai ili kufikia uchumi wa viwanda na kuongeza kipato cha familia.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu, Richard Mhina katika taarifa yake ambayo ameitoa kwa vyombo vya habari jana kuhusu maonesho hayo ambayo yatafanyika Januari 22 mwaka huu katika Chuo Kikuu cha Ushirika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Mhina alisema lengo kuu la shirika ni kuboresha maisha ya jamii masikini vijijini kwa kuongeza uzalishaji, kipato, kuboresha lishe na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.

“Tunafanya kazi na vikundi vya wakulima, taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali katika kutekeleza majukumu yetu (taasisi hizo ni makanisa, misikiti,  shule za msingi na sekondari,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema mwaka 2012 shirika lilianzisha mpango wa maonyesho ya wakulima na kushindanisha vikundi vya wakulima ili kuongeza ufanisi katika kutekeleza shughuli mbalimbali za kilimo biashara na utunzaji wa mazingira.

Kupitia mpango huu kumekuwa na mwamko mkubwa wa uzalishaji na usindikaji wa mazao ya mboga na matunda miongoni mwa wakulima wa Floresta.

Pia alisema kumekuwa na mwamko wa uoteshaji miti katika mashamba binafsi ya wakulima, pembezoni mwa barabarani, katika vyanzo vya maji, mashuleni, makanisani, na katika maeneo ya wazi kumekuwa na mwamko mkubwa katika uanzishwaji wa vitalu vya miti.

Mhina alisema wadau mbalimbali wa maendeleo wamealikwa kushiriki katika maonyesho haya ili kufikia lengo tajwa hapo juu.

“Wadau hawa ni  Serikali kuu, wizara ya kilimo, viwanda na biashara, mkoa wa Kilimanjaro, halimashauri zake, washirika wa maendeleo (FAO, Swiss Aid, Ubalozi wa Ufaransa, TOAM, SAT, NEMC, TAHA, Vyama vya kiraia, sekta binafsi, taasisi za utafiti, wasomi, viongozi wa dini, wanasiasa, wafanyabiashara na vyombo vya habari,” alisema.

Alisema wanatarajia maonesho hayo kutengeneza fursa za masoko ya bidhaa za kilimo miongoni mwa wakulima na walaji, ikihuisisha masoko ya ndani na nje ya nchi.

Alisema hiyo ni fursa kubwa kwa wasindikaji wa mazao ya mboga na matunda kufanya biashara na kujenga miundombinu imara ya uzalishaji wa malighafi zinazohitajika katika viwanda vidogo vidogo vya usindikaji.

“Kuongezeka kwa uelewa miongoni mwa wananchi juu ya umuhimu wa kufanya kilimo endelevu chenye tija ili kufikia uchumi wa viwanda

Kuanzishwa kwa viwanda vya usindikaji wa mboga na matunda hivyo kutengeneza ajira miongoni mwa wajasiriamali wadogo wadogo,” alisisitiza.

Aidha alisema maonesho hayo yatawezesha wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo pamoja na kufanya biashara

Mkurugenzi huyo alisema kupitia mpango huo wamefanikiwa kuandaa maonyesho ya shughuli zinazotekelezwa na shirika kwa miaka sita mfululizo sasa.

“Jumla ya vikundi vya wakulima vipatavyo 450 vyenye jumla ya wanachama 11,294 vimekuwa vikishiriki katika maonyesho ya kilimo na biashara na kupata fursa ya kujifunza mbinu bora za kilimo na kusindika mazao ya mboga na matunda,” alisema.

Alisema pia kupitia mpango huu, wamefanikiwa kuotesha miti takribani 1,500,000 kila mwaka kwa miaka 10 iliyopita. “Miti hiyo huoteshwa katika maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro ikiwemo vyanzo vya maji, maeneo ya wazi, pembezoni mwa barabara na katika mashamba ya watu binafsi,”alisema.

Mhina alisema taarifa za ufuatiliaji zinaonyesha asilimia 60 hadi 70 ya miti iliyooteshwa inakuwa ambapo kazi hiyo ya uoteshaji wa miti imeleta matokeo chanya katika kuboresha ikolojia  na kurejesha theluji ya mlima Kilimanjaro kwa kiasi fulani.

No comments:

Post a Comment

Pages