Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad
Masauni (kulia), akifatilia Uingizwaji wa Taarifa za Wananchi waliotoka sehemu
mbalimbali mkoani Morogoro na kufika Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya
Taifa(NIDA),zilizopo eneo la Tungi-Mfuruni mkoani hapo ikiwa ni muendelezo wa zoezi la kujipatia
kitambulisho hicho kwa wananchi nchini kote.Wapili kulia ni Afisa Usajili wa NIDA
Mkoa wa Morogoro,James Malimo.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi
Na Mwandishi Wetu
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mhandisi Hamad Masauni
amepiga marufuku watu wanaojiita mawakili na kuwatoza wananchi kiasi cha fedha kinachozidi shilingi Elfu Kumi wakidai ni ada ya kupewa nyaraka mbadala ya
cheti cha kuzaliwa ikiwa ni hitajio la msingi kwa wananchi wanaofika ofisi
mbalimbali nchini za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa(NIDA)
Akizungumza baada ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi
wa Mkoa wa Morogoro walioitaka Serikali kuweka bayana kama kupata vitambulisho
vya taifa lazima ulipe hela, Naibu Waziri Masauni alisema vitambulisho hutolewa
bure hakuna haja ya kulipa gharama yoyote huku akipiga marufuku wananchi
kutozwa fedha nje ya ofisi za NIDA
“Kuanzia sasa kila Ofisi ya NIDA itakuwa na mawakili wa
serikali wataohusika na kuandaa pamoja kuhakiki nyaraka mbalimbali za wananchi
wanaokuja kwa ajili ya vitambulisho vya taifa na ninatoa maelekezo kwa nchi
nzima katika ofisi za NIDA kuwaondoa watu wanaowaandalia wananchi nyaraka hizo
kwanza hatuwatambui kama ni maafisa sheria sahihi au la na wanaweza
kuwathibitisha watu ambao sio raia wakapata vitambulisho kama raia” alisema
Masauni
Akizungumza katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata
Ole Sanare amesema wao kama mkoa wako tayari kuleta mawakili wa serikali katika
ofisi hizo za NIDA huku akiwaasa wananchi kwenda sehemu sahihi wanapofika
kutafuta vitambulisho katika ofisi hizo.
“Serikali ipo kuhakikisha zoezi la utolewaji namba na
vitambulisho vya taifa linamalizika ndani ya siku 20 zilizoongezwa na Rais
Magufuli na kama mkoa tunayafanyia kazi maelekezo ya Naibu Waziri Masauni na
kuanzia kesho mawakili wa serikali watakuwepo hapa kuhakiki na kutengeneza
nyaraka za serikali kwa wananchi” alisema RC Sanare
Nae Afisa Usajili wa NIDA Mkoa wa Morogoro,James Malimo amesema
katika Mkoa wa Morogoro na Wilaya zake jumla ya vitambulisho 347,466 kati ya
849,436 vimezalishwa huku maombi 237.236 yakikwama kutokana na sababu
mbalimbali ikiwemo waombaji kukosa vigezo vya uraia,mihuri ya wadau na
viambata.
No comments:
Post a Comment