Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Martha Luleka akitoa ufafanuzi kwa Madiwani kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani la Sikonge la kujadili na kupitia mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2020/21.
Na Mwandishi Wetu
Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge wameiomba Ofisi ya Mkuu wa
Mkoa wa Tabora kuchunguza nia ya Polisi kutoka Mkoani kwenda katika Kijiji cha
Mpombwe na kuanza kuchukua bidhaa kwenye maduka bila Kamati ya Usalama ya
wilaya Sikonge kuwa na taarifa.
Ombi hilo la Madiwani lilitolewa
jana baada ya Diwani wa Kata ya Mpombwe Juma Mdulla kueleza tukio lilitokea
tarehe 8 Januari mwaka huu katika Kijiji hicho wakati akichangia hoja kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani la Sikonge la
kujadili na kupitia mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2020/21.
Alisema Polisi kutoka Tabora
mjini walifika katika Kijiji hicho na kwenda kwa Mwenyekiti wa Kijiji kumtaka
awaongoze kuendesha ukaguzi bidhaa zilizokwisha muda wake kwenye maduka yalipo
eneo hilo.
Diwani huyo alisema kuwa cha
kusikitisha walifanya kazi hiyo wakiwa pekee yao bila hata kuwa na wataalamu wa
Shirika la Viwango Tanzania na viongozi wengine kama Wataalamu wa sekta ya Afya
na Mtendaji wa Kata.
Aliongeza kuwa katika ukaguzi
huyo walichukua baadhi ya vipodozi na mafuta ya Petroli jambo ambalo liliacha
maswali mengi.
Mdulla alisema kuwa alipojaribu
kufuatilia juu ya taarifa za uwepo wa zoezi hilo hakupata majibu alibaini kuwa
polisi hao walifika na kuanza kazi bila hata kutoa taarifa katika Ofisi ya Mkuu
wa Wilaya ya Sikonge na wala hawakusaini Kitabu cha Wageni cha Kijiji hicho,
jambo ambalo limeacha maswali kama kweli Polisi hao walikuwa kazini au walikuwa
katika shughuli zisizo halali.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya
Wilaya ya Sikonge Peter Nzalalila alisema kitendo kilichofanywa na Polisi hata
kama kilikuwa halali walipaswa watoe taarifa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya na
kuongeza kuwa vema Mkuu wa Mkoa wa Katibu Tawala Mkoa wakapelekewa taarifa hiyo
ambayo imewasikitisha.
Alisema kumezuka tabia ya
Taasisi mbalimbali kuingia katika Wilaya ya Sikonge na kuendesha shughuli zao
na wakati mwingine kuwabughuzi wananchi bila hata kutoa taarifa kwa Mamlaka ya
Juu za Wilaya ikiwemo kwa Kamati ya Usalama ya Wilaya.
Kwa upande wa Katibu Tawala Wilaya ya Sikonge Renatus
Mahimbali alisema utaratibu unataka kabla ya Taasisi yoyote haijaanza kazi yake
ni vema ionyeshe vibali vinavyowataka kufanyakazi hiyo na watoe taarifa katika
Ofisi ya Mkuu wa Wilaya.
Alisema watu wanaoingia Sikonge na kuendesha shughuli zao
bila Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kuwa na taarifa watachukuliwa kama waharifu.
Katibu Tawala huyo wa Wilaya ya Sikonge alitoa mfano hivi
karibuni alipata taarifa kutoka kwa wananchi ya kuwepo na watu wanaodai kuandikisha
wastaafu na alipojaribu kuwahoji kwa njia ya simu na walipobaini kuwa utapeli
wao umegundulika walikata simu na kuondoka.
Aliwaomba Madiwani kuhakikisha kuwa wanapoona wageni
wanaendesha shughuli katika maeneo yao wawaombe vibali vinavyowapa ruhusa ya
kufanyakazi hiyo.
No comments:
Post a Comment