Rais Dk. John Pombe Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi
mara moja kwa aliyekuwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) katika Mkoa wa Morogoro
Mhandisi Godwin Andalwisye na wahandisi wake 12 waliokuwa na jukumu la
uangalizi wa barabara katika Mkoa huo.
Rais Magufuli ametoa
agizo hilo leo tarehe 16 Machi, 2020 baada ya kutembelea eneo la daraja la
Kiegeya lililosombwa na maji ya mvua tarehe 02 Machi, 2020 na kusababisha
kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya Dodoma – Morogoro ambayo ni kiunganishi
muhimu cha Mikoa ya Kanda ya Kati, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini
Magharibi na nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na DRC ambazo husafirisha
mizigo na abiria kwenda Dar es Salaam.
Mawasiliano ya barabara
hiyo yalirejea baada ya siku 2 na mpaka sasa eneo hilo linapitika kwa madaraja
ya muda huku kazi ya kuimarisha ikiendelea.
Rais Magufuli ameagiza
kusimamishwa kazi kwa Maafisa hao wa TANROADS pamoja na kuwachunguza kama kuna
vitendo vya hujuma walivifanya, kutokana na kutochukua tahadhari za kitaalamu
za kuzuia maji ya mvua yasisombe daraja lililokuwepo na pia kushindwa kurejesha
mawasiliano ya barabara kwa kujenga daraja haraka licha ya fedha za kufanyia
kazi hizo kuwepo.
Katika mahojiano na
Mkurugenzi wa Matengenezo wa TANROADS Mhandisi Mohamed Ntunda, Rais
Magufuli ameelezwa kuwa hadi daraja la Kiengeya linasombwa na maji ya mvua,
TANROADS katika Mkoa wa Morogoro walikuwa na zaidi ya shilingi Bilioni 3 za
matengenezo ya dharura ya barabara.
Akiwa katika eneo hilo Rais Magufuli ameliona daraja la muda lililojengwa na Wataalamu wa
TANROADS na pia ametembea kwa miguu kuelekea mto unakotirisha maji yake ambapo
ameshauri wataalamu hao waangalie uwezekano wa kujenga daraja katika eneo
jingine lenye umbali mfupi wa daraja na miinuko inayofaa endapo wataona inafaa
kufanya hivyo.
Aidha, Rais Magufuli
amemuonya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Aloyce Kamwelwe,
Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Patrick Mfugale na Mkurugenzi wa Matengenezo
wa TANROADS Mhandisi Mohamed Ntunda kutokana na kutoridhishwa na juhudi
zilizofanywa kurejesha mawasiliano ya uhakika katika eneo hilo na ametaka kosa
hilo lisirudie.
Ametoa siku 7 kwa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano pamoja na TANROADS kuhakikisha eneo hilo
linakuwa na daraja la uhakika la kupita magari kama ilivyokuwa kabla ya daraja
kusombwa na maji ili kutoathiri shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na
kukatika kwa mawasiliano ya barabara.
Rais Magufuli
amewataka Mameneja wa TANROADS wa Mikoa yote hapa nchini kuhakikisha
mawasiliano ya barabara kuu katika Mikoa yao hayakatiki vinginevyo meneja
husika atavuliwa wadhifa wake.
Wasafiri na wananchi
waliokusanyika katika eneo hilo wakati Rais Magufuli akikagua eneo hilo
wamelalamikia kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya kuelekea Hospitali ya Misheni
ya Berega kutokana na kusombwa kwa daraja, hivyo amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa
Morogoro, Loatha Sanare kuhakikisha Wakala wa Barabara za Vijijini na
Mijini (TARURA)
inajenga daraja hilo ndani ya siku 7 ili wananchi waendelee kupata huduma za
matibabu kama kawaida.
Halikadhalika wananchi hao
wamelalamikia kutokamilika kwa ujenzi wa chumba cha upasuaji katika Kituo cha
Afya Magubike na Rais Magufuli amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro
kuhakikisha jengo hilo linajengwa ndani ya miezi 2.
Pia, Wananchi hao
wamelalamikia kuchangishwa shilingi 20,000 kwa kila kaya kwa ajili ya kujenga
jengo la maabara katika shule yao ya Sekondari, lakini fedha hizo hazijulikani
zilikokwenda na badala yake wameanza kuchangishwa fedha nyingine shilingi 5,000
kwa kila kaya, na Rais Magufuli amemuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa
Morogoro Wilbroad Mutafungwa kufuatilia na kuchukua hatua stahiki.
Rais
Magufuli amechangia shilingi Milioni 5 na ameagiza wananchi wasichangishwe
fedha za ujenzi wa maabara hiyo.
No comments:
Post a Comment