HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 16, 2020

MGONJWA WA KWANZA WA CORONA AGUNDULIKA TANZANIA, WIZARA YATHIBITISHA

 
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani), kuhusu kugundulika kwa Mgonjwa wa Corona nchini, mkutano ambao ulifanyika Jijini Dar es Salaam, kulia ni Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Tigest Katsela Mangestu na kushoto ni Naibu Waziri wa Afya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, akizungumza na Waandishi wa Habari(hawapo pichani), kuhusu kugundulika kwa Mgonjwa wa Corona nchini, mkutano ambao ulifanyika Jijini Dar es Salaam, kushoto ni Naibu Waziri wa Afya  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile.

 
Na Mwandishi Wetu- MAELEZO

Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Mhe.Ummy Mwalimu imethibitisha kuwepo ka mgonjwa mmoja wa Corona ambapo amewasisitiza  wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy alisema  kuwa Machi 15, 2020 aligundulika mgonjwa mmoja mwanamke mwenye umri wa miaka 46 ambaye aliwasili na ndege ya Rwandair akitokea nchini Ubelgiji.

“Mwanamke huyu aliondoka nchini Machi 5, 2020 na alitembelea nchi za Sweden na Denmark machi 5-13 na baada ya hapo alirudi Ubelgiji na kurejea nchini machi 15, 2020, mgonjwa huyu alipita katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro, KIA na alipimwa na kuonekana hana ugonjwa huo baadae akiwa hotelini alianza kujihisi vibaya na alikwenda katika hospitali ya Rufaa Mt.Meru na sampuli ilichukuliwa na kupelekwa maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii ambapo majibu yemekuja amegundulika kuwa na Corona”, Alisema Waziri Ummy.

Alisema kuwa serikali inaendelea kuchukua tahadhari, pia aliwataka wanachi kuendelea kujikinga kwa kufuata ushauri unaotolewa na wataalamu wa Afya  wakishirikiana na Shirika la Afya duniani  WHO ili kuepuka kusambaa zaidi kwa virusi hivyo.

Aidha Waziri Ummy alisema kuwa katika Taasisi zote ambazo mikusanyiko ni mikubwa na watu kukutana mara kwa mara zikiwemo, Shule, hoteli, maduka ya biashara, nyumba za kulala wageni, makanisa, misikiti, Ofisi za Umma na Binafsi na sehemu za kutolea huduma za Afya pamoja na sehemu nyingine za mikusanyiko mbalimbali kuweka vifaa vya kunawia zikiwa na maji safi yanayotiririka na yenye Klorini.

Hatua nyingine za kujikinga ni pamoja na  kuweka maji dawa ya Klorini au vitakasa mikono, kuweka maji yenye Klorini katika vituo vya mabasi ya abiria, kuepuka kusalimiana kwa mikono, kukumbatiana, kugusa pua, mdomo pamoja na macho kadri inavyowezekana.

Waziri huyo wa Afya amezitaka hospitali zote kuhakikisha kuwa ndugu na jamaa wanaoenda kuona wagonjwa angalau wawe wawili na kutoa taarifa kituo cha Afya endepo atapatikana mtu mwenye dalili za Corona.

No comments:

Post a Comment

Pages