Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi Mary Makondo akijibu hoja kutoka kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji
mradi wa viwanja katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi akifafanua jambo wakati akijibu
hoja za baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na
Utalii wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji mradi wa viwanja katika
halmashauri ya manispaa ya ilemela mkoani Mwanza jana. Kushoto kwa Waziri ni
Mwenyekiti wa Kamati Kemilembe Lwota.
Na Munir Shemweta, WANMM MWANZA
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imevutiwa na utekelezaji mradi wa kupanga
na kupima viwanja eneo la East Buswelu katika kata ya Buswelu na Nyamhongo
halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoa wa Mwanza.
Katika utekelezaji
mradi huo, halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ilipewa mkopo usio na riba wa
shilingi Bilioni 1,550,000,000 na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
kwa ajili ya kupanga na kupima viwanja 500 na kufanikiwa kuurejesha mkopo huo kwa
wakati na kupata faida ya milioni
195,374,000.
Karibu wajumbe wote wa
Kamati hiyo waliochangia utekelezaji mradi wa viwanja katika halmashauri ya Manispaa
ya Ilemela jana wakati wa kupokea taarifa ya mradi huo walionesha kuridhishwa
na kazi nzuri iliyofanywa na watendaji wa halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi
wake John Wanga kwa kuitumia vizuri fedha waliyokopeshwa na kuzalisha faida.
Hata hivyo, Mbunge wa
Jimbo la Korogwe Timotheo Mzava alishauri faida inayopatikana kutokana na mkopo
usio na riba kwa halmashauri nchini itumike katika kazi za ardhi hasa upangaji
na upimaji badala ya kutumika katika shughuli nyingine na kutaka kuongezwa
kipengele ndani ya mkataba wa mkopo kinachoelekeza suala hilo.
Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota aliipongeza
halmashauri ya Manispaa ya Ilemela pamoja na Mbunge wake ambaye ni Naibu Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi Dkt Angeline Mabula kwa kazi nzuri ya
kuhakikisha kiasi cha fedha ilichokopeshwa kinatumika vizuri na kuleta matokeo
chanya katika halmashauri hiyo.
Kwa mujibu wa
Kemilembe, kamati yake inaunga mkono jitihada zilizofanywa na wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuzikopesha halmashauri ili kuongeza kasi ya
upimaji ardhi na kubainisha kuwa asilimia kubwa ya ardhi nchini hajapimwa na
hivyo kuchangia migogoro ya ardhi.
Kwa upande wake Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alisema utaratibu
ulioanzishwa na wizara yake wa kuzikopesha halmashauri unalenga kuongeza kasi
ya upimaji katika halmashauri mbalimbali na hivyo kuzalisha walipa kodi ya pango
la ardhi.
Amezitaka halmashauri
kutengeneza miradi ya kimkakati na
kuandika maandiko yatakayosaidia kupata
fedha za mkopo usio na riba na hivyo kuzisaidia katika shughuli zao upangaji,
upimaji na umilikishaji ardhi na
kuzalisha walipa kodi .
Aidha, Lukuvi
alibainisha kuwa, katika kuhakikisha sekta ya ardhi inafanya vizuri zaidi
Wizara yake imeanza zoezi la kuwapanga upya wataalamu wa sekta ya hiyo nchi
nzima kulingana na uhitaji sambamba na kuanzisha ofisi za mikoa ili kuondoa
changomoto za upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi nchini.
‘’Kuna baadhi ya halmashauri
zina wataalamu wengi wa sekta ya ardhi huku nyingine zikiwa na wataalamu wachache
hali hiyo inasababisha shughuli za ardhi katika halmashauri kutofanyika vizuri’’
alisema Lukuvi.
Mbunge wa Jimbo la
Ilemela Dkt Angeline Mabula alisema halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imekuwa
ikifanya vizuri katika zoezi la upangaji, upimaji na umilikishaji ardhi na
katika kipindi cha miaka miwili imefanikiwa kupunguza migogoro ya ardhi kwa
kiasi kikubwa na kutoa hati 22,185.
Kwa upande wake Katibu
Mkuu Wizara ya Ardhi nyumba na maendeleo ya Makazi Mary Makondo alisema wizara
yake imejipanga kuhakikisha inakabiliana na changamoto ya watumishi kwa
kuwapanga katika mikoa yote ishirini na sita ya Tanzania Bara.
Kwa mujibu wa Mary, katika
kipindi hiki ambacho idadi ya wataalamu wa sekta ya ardhi hawatoshelezi halmashauri
zenye miradi zinaweza kutumia wataalamu kutoka halmashauri nyingine ili kuharakakisha
kazi na hivyo kuongeza kasi ya upangaji na upimaji katika maeneo mbalimbali.
No comments:
Post a Comment