HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

March 17, 2020

Kamati yawahakikishia ajira wakazi Mbagala

 Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, akimuonesha Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso na Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Miraji Mtaturu (Kushoto) moja ya nondo katika
miundombinu iliyoanza kujengwa ya mabasi ya yaendayo haraka (BRT), wakati kamati hiyo ilipotembelea mradi huo, jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso, akizungumza na wananchi wa maeneo ya Mbagala, mara baada ya
kupokea maombi yao ya kupewa kipaumbele katika mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT), ya awamu ya pili, mara baada ya kamati hiyo kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo, jijini Dar es
Salaam.
Muonekano wa hatua iliyofikiwa ya moja ya vituo vya mabasi yaendayo haraka (BRT) awamu ya pili, eneo la DUCE jijini Dar es Salaam. Awamu hiyo itahusisha ujenzi wa vituo vya mabasi 29, vituo vikuu vya mabasi (Terminals) 2 na vituo mlisho viwili (2), daraja moja la waenda kwa miguu, ujenzi wa karakana (Depot) 1, barabara yenye urefu wa kilometa 20.3 na Flyovers mbili (2).


Na Suleiman Msuya

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imewahikikishia ajira wananchi wa maeneo ya Mbagala katika Mradi wa Ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT) kwa awamu ya pili unaoendelea kutekelezwa jijini Dar es Salaam.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso, wakati aliposimamishwa na wananchi wa maeneo hayo wakati kamati hiyo ilipokuwa ikikagua ujenzi wa mradi huo unaotekelezwa na mkandarasi Synohydro Corporation kutoka china kwa muda wa miezi 36.

Kufuatia maelezo ya wananchi hao, Mwenyekiti huyo ameiagiza Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wakala wa Barabara (TANROADS) mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha wanasikiliza kero za wananchi hao ili kuwe na usawa kwenye ajira ambazo zinatolewa kwa wazawa.

"Kilio chenu tumekipokea na sisi kama Kamati tunatoa agizo kwa msimamizi wa mradi kulisimamia hili kwa haki na usawa kwani huu mradi ni wa kitaifa na ndo umeanza", alisisitiza Kakoso.

Akitoa wito kwa wananchi waliopo maeneo jirani na miradi yote inayoendelea kutekelezwa nchini kulinda na kuthamini miradi hiyo kwa kutojihusisha na vitendo vya uhujumu wa miunbombinu kwa kuiba mafuta na vifaa vya ujenzi.

"Watanzania mkipewa kazi kwenye miradi itunzeni iyo heshima mliyopewa kwa kutoshiriki katika matukio ya wizi wa mafuta, saruji na vitu vingine visivyopendeza", alisema Kakoso.

Kuhusu suala la utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa awamu ya pili ya miundombinu ya BRT, Kamati imeipongeza Serikali kwa hatua iliyofikiwa na wataalamu wa ujenzi wa miundombinu hiyo yenye lengo la kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.

Alitaka TANROADS kumsimamia mkandarasi vizuri ili aweze kukamilisha miundombinu hiyo kwa muda uliopangwa.

"Tunajua kuwa kila siku idadi ya watu inaongezeka hivyo tunahitaji miundombinu imara ambayo iko salama ili itufikishe kwenye uchumi wa kati", alisema Mwenyekiti huyo.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Hawa Mchafu, aliishauri TANROADS kutoelekeza mifereji ya maji katika makazi ya watu ili kunusuru uhabirifu wa mazingira na mali zao.

Mmoja wa wajumbe wa Kamati hiyo, Zuberi Kuchauka ambaye ni  Mbunge wa Jimbo la Liwale, amewataka wataalamu wa usanifu wa miradi ya barabara nchini kutumia taarifa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kupanga vizuri namna ya kuboresha miundombinu hiyo kwa kuwa na madaraja makubwa na makalvati sehemu husika.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Elias Kwandikwa, ameihakikishia kamati hiyo kutekeleza maelekezo yote yaliyoelekezwa kwa Wizara na TANROADS na kuusimamia mradi wa BRT kwa viwango na ubora.

Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), Mhandisi Crispianus Ako, ameieleza kamati hiyo kuwa ujenzi wa mradi huo unahusisha  barabara yenye urefu wa kilometa 20.3, Flyovers mbili (2),  vituo vya mabasi 29, daraja moja la waenda kwa miguu, ujenzi wa karakana (Depot) 1, vituo vikuu vya mabasi (Terminals) 2 na vituo mlisho viwili (2).

Ujenzi wa Miundombinu ya usafiri wa haraka wa mabasi (BRT), awamu ya pili unahusisha barabara ya Kilwa (Kamata hadi Mbagala), barabara ya  Chang'ombe/Kawawa (Magomeni hadi Mgulani) na barabara ya Sokoine (Gerezani - City Hall).

No comments:

Post a Comment

Pages