Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdoun Mansoor akiwaonesha ramani Wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii eneo la mradi wa
upangaji na upimaji ardhi katika manispaa ya Shinyanga jana wakati wa kukagua
mradi huo mkoani Shinyanga. Katikati anayeangalia ramani hiyo ni Mwenyekiti wa
Kamati Kemilembe Lwota.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kemilembe
Lwota akitoa maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga
Geofrey Mwangulumbi (aliyevaa Kaunda suti) wakati Kamati yake ilipokwenda
kukagua mradi wa upangaji na upimaji ardhi katika manispaa hiyo jana mkoani
Shinyanga.
Na Munir Shemweta, WANMM SHINYANGA
Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Malisili na Utalii imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa
kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika Halmashauri ya Manispaa ya
Shinyanga mkoani Shinyanga.
Mradi huo wa viwanja
320 ni mkopo usio na riba wa shilingi milioni 240 kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi kwa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga ukiwa na lengo
la kuongeza kasi ya upangaji, upimaji na umilikishaji ili kuondoa migogoro ya
ardhi.
Akizungumza wakati wa
ziara ya kukagua mradi huo mkoani Shinyanga jana Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Kemilembe Lwota alisema kamati yake
imeridhishwa na mradi huo na kuuita wa mfano
kwa kuwa umetekelezwa kwa asilimia mia moja.
Kwa mujibu wa Kemilembe,
kati ya halmashauri 24 zilizopatiwa mkopo wa aina hiyo halmashauri nne zimerejesha
fedha zilizokopeshwa kwa asilimia mia moja na baadhi yake zimepata faida kupitia
mkopo huo ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga na kuzitaka halmashauri
nyingine kwenda kujifunza katika Manispaa hiyo.
‘’Sote tunajua migogoro
ya ardhi iliyopo Tanzania na tumekuwa tukihimiza kwa muda mrefu upangaji,
upimaji na umilikishaji maeneo ili kuondoa migogoro na nia ya kamati yetu ni
kutaka kuona kila kipande cha ardhi kinapimwa’’ alisema Kemilembe
Aliipongeza Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa hatua kubwa ya kutoa fedha za mkopo usio
na riba kwa halmashauri ili kuongeza kasi ya upangaji ambapo alitoa wito kwa
wananchi kununua maeneo yaliyopimwa na kumilikishwa kwa kuwa hati zake zinaweza
kutumika kuchukulia mkopo benki.
Kwa upande wake Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema pamoja na mamlaka ya upangaji kuwa
chini ya halmashauri lakini Wizara yake iliamua kuziwezesha baadhi ya
halmashauri kwa kuzipatia mkopo wa fedha usio na riba ili kuongeza kasi ya
upangaji, upimaji na umilikishaji maeneo.
Amezitaja halmashauri zilizopatiwa
mkopo katika mkoa wa Shinyanga mbali na Manispaa ya Shinyanga kuwa ni halmashauri
ya Mji wa Kahama milioni 220 na ile ya Mji wa Msalala milioni 120 ambazo zote zimefanikiwa
kurejesha mikopo yake kwa asilimia mia moja
‘’ Lengo la Wizara ya
ardhi ni kupanga, kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini na mkopo tunaoutoa
sasa kwa baadhi ya halmashauri unatokana na upatikanaji fedha ‘’ alisema Dkt
Mabula.
Hata hivyo, Naibu
Waziri Mabula alisema, Wizara yake katika siku zijazo ina mpango wa kupima kila kipande cha ardhi kutokana na
Benki ya Dunia na ile ya Exim-Korea kuonesha nia ya kusaidia zoezi hilo na
kusisitiza kuwa suala hilo litakapofanikiwa migogoro ya ardhi nchini itapungua
kama siyo kuisha kabisa.
No comments:
Post a Comment