Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wadau wa Elimu wa Wilaya ya
Ruangwa, mkoani Lindi, kwenye kikao cha maendeleo ya elimu,
kilichofanyika katika ukumbi wa Narung’ombe, Machi 14, 2020. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa shule zote nchini wahakikishe
wanaendelea kutekeleza agizo la Serikali la kudhibiti michango holela
kwenye shule zao.
Amesema
lengo la elimu msingi bila ada ni kuleta ujumuishi kwa watoto wote
hususani wale wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo wapate fursa
ya kusoma.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Machi 14, 2020) wakati
akizungumza na wadau wa elimu wilayani Ruangwa kwenye kikao
kilichofanyika katika ukumbi wa Narung’ombe.
Amesema
sekta ya elimu ndio wakala wa mabadiliko ya kiuchumi, kiteknolojia na
kijamii katika nchi yoyote, hivyo ni muhimu ikapewa kipaumbele kwa
maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla.
Pia,
Waziri Mkuu amesema ili sekta hiyo iweze kupata mafanikio tarajiwa ni
lazima wazazi na walezi nao washiriki kikamilifu katika kufuatilia
mienendo ya watoto wao kwa kuhakikisha wanakwenda shule badala ya
kuliacha jukumu kwa walimu pekee.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amewapongeza walimu wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa
bidii waliyokuwanayo katika utendaji kazi hali iliyowezesha wilaya kuwa
na matokeo mazuri katika mitihani mbalimbali ya Kitaifa.
“Kazi
mnayofanya inaonekana, nawasihi muendelee hivi hivi na wilaya yetu
itaweza kuendelea kupiga hatua kielimu. Pia muwaelimishe wazazi na
walezi juu ya umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya vijana wetu.”
Akizungumzia
kuhusu, homa ya mapafu inayosababishwa na virusi vya corona, Waziri
Mkuu amewasisitiza wadau hao wa elimu wakiwemo walimu kwenda
kuwaelimisha wanafunzi na wananchi namna ya kujikinga na virusi hivyo
ikiwa ni pamoja na kutosalimiana kwa kushikana mikono.
Kwa upande wake,
Afisa Elimu (Sekondari) wilaya ya Ruangwa Mwalimu Ernest Haule amesema
katika mwaka masomo wa 2020 asilimia 86 ya wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza waliripoti katika shule walizopangiwa.
Akizungumzia
kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya elimu wilayani Ruangwa amesema
ni pamoja na upungufu wa walimu, vyumba vya madarasa, nyumba za walimu
pamoja na utoro kwa wanafunzi.
Naye,
Afisa Elimu Mkoa wa Lindi, Vicent Kayombo amewapongeza wadau wa elimu
kwa ushirikiano wao uliosababisha wilaya ya Ruangwa kufanya vizuri
katika mitihani mbalimbali ngazi ya Taifa.
Amesema
baada ya kuona wadau wa wilaya hiyo wakiongozwa na Halmashauri
wameanzisha utaratibu wa kugawa zawadi kwa walimu na wanafunzi
waliofanya vizuri waliagiza halmashauri zote mkoani Lindi kuiga
utaratibu huo wa kuwatambua waliofanya vizuri.
Waziri
Mkuu ameungana na uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa
kugawa zawadi kwa walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika mitihani
ya Kitaifa ya kidato cha sita, nne na darasa la saba.
No comments:
Post a Comment