Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
Chama cha Waandishi wa Habari Wananawake (TAMWA Zanzibar)
kimewaomba na kuwashauri wanawake wa vyama vyote kuhakikisha wanajitokeza
kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo.
Ombi hilo limetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa chama hicho Dt.
Mzuri Issa Ali kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo
Visiwani Zanzibar.
Alisema kuwa Kwa mujibu wa Sensa ya idadi ya watu na makaazi
ya mwaka 2012 Zanzibar ina idadi ya watu wapatao 1,303,569 na kukisiwa kufikia 1,671,598
kwa mwaka 2020 ambapo wanawake ni zaidi ya asilimia 50.
“Hata hivyo uwingi huo wa wetu hauendani na katika vyombo vya kutunga sheria na kufanya
maamuzi na tuliowengi huvunjwa moyo na kupikiwa majungu kwa makusudi wakati wa
kugombea nafasi hizo ili hali hiyo isibadilike” alisema Dt. Mzuri.
Alifahamisha kwamba Kutokana na mazingira hayo, ni wastani
wa wanawake 200 tu ndio walioteuliwa na vyama vyao kwa Zanzibar kugombea katika
maeneo hayo matano ya uchaguzi ya mwaka 2015 ambapo kwa nafasi ya Uraisi iliendelea
kutokuwa na mwanamke tokea kurejea kwa vyama vingi.
“ tunawaomba wanawake wajitokeze kwa wingi kutumia haki yao
ya kikatiba na pia kuwaongoza wananchi katika nafasi mbali mbali sambamba na
wenzao wanaume” alieleza.
Alieleza pia Imekuwa ni kawaida, wanawake kuelekezwa
kugombea katika viti maalum tu ambavyo kijinsia huwa havioneshi usawa wa
kijinsia na umoja wa wanawake bali huchangia kwa kiasi kikubwa kuleta
mgawanyiko wa wanawake.
“Katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2015 ni wanawake watatu tu ndio walioweza kuchaguliwa
kupitia kwenye majimbo katika nafasi za ubunge sawa na asilimia 6, wawakilishi
saba sawa na asilimia 14, madiwani 23 sawa na asilimia 20 na nafasi ya Uraisi
ambayo ni moja tu imeendelea kushikiliwa na mwanamme” alieleza Mzuri kupitia
taarifa hiyo kwa waandishi wa habari.
Sambamba na hilo TAMWA Zanzibar inaishauri jamii kuwaunga
mkono wagombea wanawake ili waweze kuonesha uwezo wao na hivyo kuleta uwiano
katika jamii pamoja na maendeleo kwa ujumla.
Wakati huohuo waliiomba Tume ya Uchaguzi (ZEC) kuweka mfumo maalum wa
kupokea maoni kutoka kwa wananchi hasa wanawake wanaokumbwa na udhalilishaji
katika kipindi hichi cha heka heka za uchaguzi.
No comments:
Post a Comment