Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, (katikati), akiwa
katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Pwani. Kushoto kwake
ni Mbunge wa Jimbo la Kibaha mjini,
Silvestry Koka kabla ya kwenda kufunga kambi ya wagonjwa wa corona katika eneo
la Lulanzi Wilayani Kibaha. (Picha na Victor Masangu).
NA
VICTOR MASANGU, KIBAHA
WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii na
Wazee Ummy Mwalimu amefunga kambi ya wagonjwa wa Corona iliyokuwa Lulanzi
Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani.
Akifunga kambi hiyo jana
ambapo alisema, kati ya kambi 85 zilizokuwa zinahudumia wagonjwa wa
Corona zimebaki 11 ambazo nazo zinaendelea kufungwa siku zijazo kutokana na
ugonjwa huo kuendelea kutokomea hapa nchini.
Aliwasihi wananchi kuacha
kujibweteka na kuendelea kuchukua tahadhari ya ugonjwa huo katika maeneo
mbalimbali ili kuepuka kupata maambukizi mapya.
"Tumefunga kambi 74 hadi sasa
na hii hapa Lulanzi ilikuwa ni Kati ya kambi kubwa ambayo ilikuwa inapokea
wagonjwa wengi na leo naifunga rasmi kwani mgonjwa wa mwisho hapa aliruhusiwa
Mei 26 hakuna mwingine aliyepokelewa hadi leo" alisema
Aidha Waziri Ummy aliwataka wakazi
wa Kibaha kufika katika Hospitali ya Wilaya kupata huduma na kuondoa hofu ya
kuwa kituoni hapo bado kuna wagonjwa wa Corona.
Alisema, wananchi wanatakiwa kuondoa
hofu kwani majengo yote yamefanyiwa usafi baada ya wagonjwa kuondoka katika
Hospitali.
" Lulanzi sio tena kambi ya
wagonjwa wa Corona , wananchi ondoeni wasiwasi na mfike kupata huduma za afya,
tusikimbilie Tumbi ile ni Hospitali ya Rufaa tungependa ibaki kutoa huduma za
hadhi ya Rufaa" alisema Ummy.
Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito
kwa Halmashauri ya mji wa Kibaha kusimamia utoaji wa huduma za viwango
vinavyostahili kwa wagonjwa.
Akiongea katika Hospitali hiyo
Mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alimshukuru Rais Pombe Magufuli
kwa Hospitali hiyo ambayo imemaliza uhitaji wa Hospitali ya Wilaya aliyokuwa
akiiomba kwa zaidi ya miaka saba iliyopita.
Koka aliwataka wananchi kufika
kutibiwa katika Hospitali hiyo ambayo imeondoa kilio cha uwepo wa Hospitali ya
Wilaya .
Alisema changamoto iliyopo katika
Hospitali hiyo kwasasa ni pamoja na ubovu wa barabara na gari la wagonjwa
ambalo Waziri Ummy aliahidi litapatikana hivi karibuni.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya mji wa
Kibaha Tulitweni Mwinuka alisema, Hospitali hiyo imeanza kutoa huduma za
kawaida kwa wagonjwa Juni 6 na kwamba jamii bado ina Mashaka kufika katika
Hospitali hiyo.
No comments:
Post a Comment