Na Janeth Jovin
RAIA wawili wa Kenya na Watanzania wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka ya uhujumu uchumi ikiwemo kuisababisha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), hasara ya Sh milioni 16.6.
Washitakiwa hao ni Beth Ngunyi (43) mfanyabiashara na Mkazi wa Kasaram Nairobi, Frolence Dirango (34) mfanyakazi wa Kampuni ya Betlee kama Ofisa wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Alven Swai (26) mkazi wa Mbezi Beach na Godluck Macha (28) mfanyabiashara na Mkazi wa Mbezi beach.
Akisoma hati ya mashtaka mahakamani hapo leo, Wakili wa Serikali, Batilda Mushi amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Yusto Ruboroga kuwa kati ya Julai Mosi na Julai 26, mwaka huu katika maeneo mbalimbali, washtakiwa kwa pamoja walikula njama ya kutumia vifaa vya mawasiliano.
Amedai Julai 13, mwaka huu maeneo ya Tarakea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, Ngunyi na Dirangu waliingiza vifaa vya kielekroniki nchini pasipo kuwa na leseni ya TCRA.
Mushi amedai Julai 20, mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, washtakiwa hao walisimika vifaa vya mawasiliano bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Katika shtaka la nne, imedaiwa kati ya Julai 20 na 26, mwaka huu maeneo ya Kibona lodge Mbezi beach, kinyume na sheria walifanyia marekebisho ya vifaa hivyo vya kielektroniki.
Pia imedaiwa kinyume na sheria washtakiwa hao waliendesha mitambo ya mawasiliano bila kuwa na leseni kutoka TCRA.
Aidha Mushi amedai kinyume na sheria washtakiwa hao walitumia vifaa vya mawasiliano vilivyounganishwa na vifaa vingine vya mawasiliano kwa nia ya kupokea na kusambaza mawasiliano bila kupata uthibitisho wa TCRA.
Washtakiwa hao wanadaiwa walikwepa kufanya malipo ambayo yalipaswa kufanyika kwa kuruhusu mawasiliano nje ya nchi kutokana na kutumia kifaa hicho cha mawasiliano bila kuwa na leseni.
Katika shtaka la tisa, imedaiwa Julai 13, mwaka huu maeneo ya Kibona Lodge, Mbezi beach, washitakiwa Ngunyi na Dirangu wanadaiwa kuwepo nchini bila kuwa na kibali.
Mshtakiwa Macha amedaiwa Julai 15, mwaka huu kinyume na sheria aliwahifadhi Ngunyi na Dirangu kuishi kwenye Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wakijua hawana kibali.
Katika shtaka la 11, imedaiwa kati ya Julai 20 na 26, mwaka huu maeneo ya Kibona lodge Mbezi beach jijini Dar es Salaam washitakiwa hao waliisababishia TCRA hasara ya Sh 16,634,400.
Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Ruboroga aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa wote wamerudishwa rumande kwa sababu mashitaka hayo hayana dhamana labda watakapoomba Mahakama Kuu.
No comments:
Post a Comment