Na Victor Masangu Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo ameingilia kati sakata sugu lililodumu kwa kipindi cha miaka mingi la mapigano ya wakulima na wafugaji na ambapo amelitafutia ufumbuzi wa kudumu baada ya kuagiza kuanzia sasa mifugo yote iliyopo katika bonde la mto Ruvu kuondolewa mara moja na kupelekwa katika maeneo mengine maalumu ambayo yametengwa na serikali kwa ajili ya marisho na kuagiza wafugaji walioingiza mifugo yao mashambani wakamatwe wote.
Ndikilo alitoa agizo hilo wakati akizungumza na wananchi wa vijiji mbali mbali vilivyopo katika Tarafa ya Ruvu Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani ikiwa ni utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Waziri mkuu wakati alipofanya ziara yake ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) katika eneo la Ruvu ambapo alibaini kuwepo kwa kero na changamoto nyingi zinazowakabili wananchi hao.
Pamoja na kuwapiga marufuku hiyo, lakini pia amemuagiza kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani Wankyo Nyigesa,kuhakikisha wanaendesha oparesheni ya kila siku katika bonde hilo na mfugaji atakayekamatwa achukuliwe hatua kali.
Hatahivyo,Ndikilo tayari ametoa amri ya kukamatwa kwa baadhi ya wafugaji akiwemo Daudi Masanja na Sauti Mbili ambao wamekuwa na kiburi cha kulisha kwa makusudi mifugo yao kwenye mashamba ya wakulima wa bonde la Mto Ruvu.
Wafugaji hao wanadaiwa kuingiza mifugo yao katika mashamba ya wakulima wa Kijiji cha Minazi Mikinda kilichopo Kata ya Ruvu Wilayani Kibaha na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh.milioni 50 ambapo wametakiwa kulipa fedha hizo ndani ya wiki moja.
Ndikilo,alitoa kauli hiyo katika mkutano wake wa kusikiliza kero za wananchi wa Kijiji cha Minazi Mikinda kilichopo Kata ya Ruvu Wilayani Kibaha ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Agosti 7 mwaka huu alipokuwa akitembelea mradi wa reli ya mwendokasi(SGR) uliopita Kijijini humo.
Katika mkutano huo Ndikilo,akiwa na kamati ya ulinzi na usalama alipokea kero 34 za Wananchi lakini kero kubwa ilikuwa juu ya migogoro kati ya wakulima na wafugaji jambo ambalo lilimchukiza na kuanza kukunjua makucha na kuchukua hatua kali dhidi ya wafugaji hao.
Ndikilo,alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya mifugo imetenga eneo la ekari 20,000 katika Ranchi ya Ruvu na kuanzia sasa wapeleke mifugo yao katika eneo hilo na hakuna ruhusa ya kuingiza mifugo yao katika bonde la mto Ruvu na mfugaji atakayekiuka atakiona.
Alisema,mfugaji yeyote aliyeingiza mifugo yake katika mashamba ya wakulima na wale waliofanya vurugu ya kuhatarisha maisha ya wakulima watakamatwa ili wachukuliwe hatua za kisheria na kwamba hakutakuwa na huruma katika hilo.
Ndikilo, alisema wakati mwingine watendaji wa Vijiji ,Kata,Wilaya na maofisa wengine wa Serikali wamekuwa wakishirikiana katika kuwalinda wafugaji jambo ambalo ni baya kwakuwa linadhurumu haki za wakulima huku akisema kwasasa mtendaji wa namna hiyo nae lazima ashughulikiwe.
"Nimekuja na sindano yenye dawa ya kutibu ugonjwa wa Minazi Mikinda na kuanzia sasa bonde la Mto Ruvu litabaki kuwa la wakulima kwa ajili ya kujitafutia kipato na ole wake mfugaji akamatwe na mifugo yake kwenye bonde hilo atakiona,"alisema Ndikilo.
Nao baadhi ya wakulima hao akiwemo Mohamed Telemkeni, alisema kuwa mpaka sasa ni siku ya saba anaogopa kwenda shambani kwake kwakuwa ametishiwa kuuawa na wafugaji .
Telemkeni ,alisema kuwa yeye hulima mbogamboga katika bonde hilo lakini kutokana na hali hiyo maisha yake yamekuwa magumu kwakuwa mazao aliyokuwa akitegemea yameliwa na Ng'ombe na hivyo kuishi kwa shida.
Nae Abdallah Mapunda,alisema amelima ekari 40 lakini mazao yote yameliwa na Ng'ombe ambapo ameiomba Serikali ifanye msako wa kukamata Ng'ombe wote wanaongia katika mashamba ya wakulima.
Siku tatu zilizopita Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa alipokuwa katika ziaara yake ya kikazi ya siku moja ya kutembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) Katika eneo la ruvu Wilaya ya Kibaha alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani kushughulikia kero na chanagmoto zote zinawazokabili wananchi wa maeneo hayo ikiwemo mgogoro wa wakulima na wafugaji.
No comments:
Post a Comment