Mtaalam Kijana wa Kimataifa Anayeshughulikia Ufuatiaji na Thamani wa
Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu FORVAC), Nette
Korkanen akipokea zawadi ya begi kutoka kwa wanachama wa Kikundi cha
Tumeamua cha Kijiji cha Ukata wilayani Mbinga mkoani Ruvuma.
NA SULEIMAN MSUYA, MBINGA
KIKUNDI
cha Tumeamua kilichopo kijiji cha Ukata, Kata ya Ukata wilayani Mbinga
mkoani Ruvuma kimeomba Program ya Mnyororo wa Thamani wa Mazao ya Misitu
(FORVAC) kuwasaidia shilingi milioni 15 ili kukuza mtaji wa kikundi.
Ombi
hilo limetolewa na Katibu wa kikundi hicho Erasto Nchimbi wakati
akisoma risala mbele ya waandishi wa habari waliotembelea kijiji hicho
kuona shughuli za Program ya FORVAC wilayani Mbinga.
Amesema kikundi cha Tumeamua kimeanzishwa mwezi Machi 2020 kikiwa na wanachama 25 ambapo wanaume 19 na wanawake 6.
Nchimbi
amesema baada ya miezi saba ya kujenga kikundi baadhi ya wanachama
walikata tamaa na hivi sasa kikundi kina wanachama 11 ambao
wanatengeneza bidhaa zitokanazo na zao la mianzi inayopatikana kwenye
Msitu wa Hifadhi ya Namswea-Lilengalenga kijijini hapo.
Amesema
wamelazimika kuomba msaada wa shilingi milioni 15 ili kuhakikisha kuwa
lengo la FORVAC la kutaka wanavijiji kutunza na kutumia rasilimali
misitu kwa njia endelevu ili kujiendeleza linatimia.
"Shilingi milioni 15 zitaweza kutusukuma mbele kwani shughuli zetu za ususi zinahitaji mtaji wa uhakika ili kufikia soko kubwa.
Baadhi
ya bidhaa tunazotengeneza kutokana na mianzi kutoka msitu wa
Namswea-Lilengalenga ni nyungo, majamanda, mabegi ya akina mama, fagio,
viti, mikeka, chujio ya nazi, vitanda, masanduku na mapambo," amesema.
Amesema
kupitia fedha hizo wanatarajia kutengeneza bidhaa za sofa, meza, kabati
na nyingine kwa kutumia mianzi ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi.
Katibu
huyo ametaja changamoto wanayokabiliana nayo kuwa ni pamoja na kukosa
eneo la kutengenezea bidhaa hali ambayo inachangia wakae chini ya
mwembe.
Changamoto
nyingine ni ukosefu wa usafiri wa kusafirishia malighafi kutoka msituni
na vitendea kazi duni hivyo kukwamisha baadhi ya shughuli.
Aidha,
amesema wanakabiliwa na changamoto ya elimu na masoko ya uhakika ya
bidhaa zao hivyo wanaomba FORVAC waendelee kuwasaidia ili kutimiza lengo
la kikundi.
Akizungumzia
ombi hilo Mratibu wa FORVAC Kongani ya Ruvuma, Marcel Mutunda amesema
ombi hilo linafanyiwa kazi na Program na ni matumaini yao watawapatia
msaada huo wa kukuza kikundi.
Mutunda
amesema matamanio yao ni kuhakikisha wanavijiji wanaozungukwa na misitu
wanapata faida ya kiuchumi, kimazingira, kijamii na maendeleo huku
uhifadhi endelevu ukionekana.
Amesema
kikundi cha Tumeamua kimeonesha matumaini kwa muda mchache hivyo
wanapaswa kuungwa mkono ili kuhakikisha msitu unakuwa salama.
"FORVAC
tuliitisha maandiko ambapo Kikundi cha Tumeamua kiliomba na ombi lao
wamepita hatua ya kwanza hivyo ni matumaini yangu watapata msaada huo.
Ila fedha hazitakuja kabla ya kupata elimu ambapo FORVAC wameingia
makubaliano na Shirika la Sedit- Vicoba lenye makao makuu yake Jijini
Dar Es Salaam ambao watatoa mafunzo kwa kikundi katika eneo la masoko.
Pia
tumewasiliana na mtaalam wa ufundi kutoka Kampuni ya Emmanuel ya
iliyoko Uyole, Mbeya ili aje kuwajengea uwezo kielimu," amesema.
Mutunda
amesema ili kuhakikisha kuwa mradi unakuwa endelevu wamehamasisha
wanakikundi kupanda miti ya mianzi ili baadae waweze kuitumia.
Aidha,
amesema wamesukumwa kuhamasisha ususi katika Kijiji cha Ukata kwa
sababu historia inaonesha tangu zamani hizo kijiji kilikuwa na wasusi na
kwamba vijiji vingine vya Amani-Makolo , Kiwombi,Kindimba juu, Kindimba
chini, Barabara Ndongosi vinajishughulisha na ufugaji nyuki na uvunaji
uyoga kutoka msituni.
No comments:
Post a Comment