BAADHI ya Wananchi wa Shehia za Mchikichini na Hawai wakifanya usafi katika maeneo yao kwa kushirikiana na viongozi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi 'A' na Viongozi wa Jimbo la Welezo. (PICHA NA IS-HAKA OMAR).
MBUNGE wa Jimbo la Welezo Mhe.Maulid Saleh Ali (kulia) akisukuma bero la taka kwa ajili ya kwenda kuzihifadhi katika eneo maalum la taka, katika zoezi la usafi wa mazingira lililofanyika leo katika Shehia za Hawai na Mchikichini ndani ya Jimbo la Welezo Zanzibar.
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MBUNGE wa Jimbo la Welezo Mhe.Maulid
Saleh Ali,amewataka wananchi wa jimbo hilo kuendeleza utamaduni wa
kufanya usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuepuka maradhi ya
miripuko.
Wito huo ameutoa leo mara baada ya kushiriki kampeni
maalum ya usafi wa mazingira iliyofanyika katika shehia za Hawai na
Mchikichini jimboni humo alisema kila mwananchi ana jukumu la kufanya
usafi katika eneo analoishi ili kudumisha dhana ya usafi kwa vitendo.
Alisema
kwa kushirikiana na uongozi wa jimbo atahakikisha suala la usafi
linapewa kipaumbele kinachositahiki ili shehia zote ziwe safi muda wote.
Aliahidi
kwamba atatoa vifaa vya kisasa vya kusafisa mazingira vikiwemo
mifagio,mapanga na ndoo maalum za kuifadhia takataka ili kuweka
mazingira ya jimbo hilo katika hali ya usafi.
Pamoja na hayo
aliwasihi vijana mbalimbali wa jimbo hilo kuanzisha vikundi vya kufanya
usafi ili visaidie kufanya usafi sambamba na kulinda mazingira ya jimbo
hilo yasiharibiwe.
''Wito wangu kwa wananchi wote wa Jimbo hili
ni kwamba kila mtu kwa nafasi yake bila kujali cheo na wadhifa wake sote
tushirikiane katika kufanya usafi wa mazingira kwani faida ya kufanya
hivyo ni kubwa zaidi kuliko kuacha kila eneo likatupwa taka.'', alisema
Maulid.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa ya Magharibi
''A'' Amour Ali Abdallah,amesema kwa upande wa manispaa hiyo wamejipanga
kushirikiana na masheha mbalimbali kutoa elimu kwa wananchi juu ya
umuhimu wa kudumisha usafi na ulinzi wa mazingira.
Alisema pamoja
juhudi za shehia hiyo ya Hawai kuandaa siku maalum ya ''shehia day''
kwa ajili ya kuhamasisha masuala ya usafi katika maeneo hayo bado
wananchi hawajahamasika kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa
kampeni hiyo.
Alisema shehia mbalimbali za manispaa hiyo
zinakabiliwa na tatizo la ukosefu wa maeneo maalum ya kutupa takataka
jambo ambalo litafutiwa ufumbuzi wa kudumu na manispaa hiyo.
Aidha
Kaimu Mkurugenzi huyo Amour, alisema kampeni hiyo ya kufanya usafi wa
maeneo mbalimbali ya shehia hizo unatakiwa kuwa endelevu na kuzitaka
shehia zingine za manispaa hiyo kuiga kwani ni utaratibu mzuri unaosaidi
kuweka mazingira katika hali ya usafi.
Alisema Manispaa hiyo
itaanza zoezi la kukagua usafi nyumba kwa nyumba na wananchi
wakaobainika wanaishi katika mazingira machafu watatozwa faini sambamba
na kuchukuliwa hatua kali za kisheriA.
''Mheshimiwa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi,
anasisitiza nchi iwe katika hali ya usafi sasa na sisi lazima katika
ngazi zetu tutekeleze agizo hilo kwa kuhakikisha mitaa yote na maeneo
mbalimbali ya manispaa yetu yanakuwa safi muda wote.'', alisisitiza
Amour.
Naye Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Choum Shuwari
Machano,aliwapongeza wananchi waliojitokeza kushiriki katika zoezi hilo
la usafi ambalo linagusa maisha ya kila mwananchi.
Aliwasihi
wananchi hao kuendeleza utamaduni wa kufanya usafiri katika maeneo yao
bila ya kusubiri watendaji wa Manispaa kwani suala la usafi
linawahusisha watendaji wote.
Akizungumza Sheha wa Shehia ya
Mchikichini Kijakazi Ferouz Khamis,alisema wanaendelea kuwahamasisha
wananchi wajitokeze kwa wingi kufanya usafiki katika maeneo yao.
Naye
Mkaazi wa Shehia hiyo Asha Seif Salum, aliomba Manispaa ya Magharibi
''A'', kufanya kutenga maeneo maalum ya kutupa taka ili kuepusha taka
hizo kusambaa mitaani.
No comments:
Post a Comment