NA DENIS MLOWE, IRINGA
MBUNGE wa jimbo la Kilolo mkoani Iringa, Justin Nyamoga amesema atahakikisha ndani kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake wanakijiji cha Mgoweko kilichoko kata ya Nyanzwa wilaya ya Kilolo wanapatiwa umeme
Akizungumza wakati wa mkutano wa kuwashukuru wananchi kwa kumchagua kuwa mbunge uliofanyika katika kijiji cha Mgoweko, Nyamoga alisema kuwa kitendo cha wananchi hao kukipatia kura za kutosha chama cha Mapinduzi katika uchaguzi mkuu kimewapa deni kubwa la kuhakikisha wanaleta maendeleo.
Alisema kuwa kura za kishindo alizopata rais na wabunge zimekuwa deni kubwa kwao hivyo watahakikisha ndani ya kipindi cha miaka mitano vijiji hivyo vinapata umeme wa REA kwani atasimamia hilo kwa karibu zaidi.
“Ndani ya hii miaka mitano nitahakikisha kwamba tunashirikiana katika kutatua kero ambazo zipo zinatatuliwa na wananchi wanaendelea kuwa na maisha bora zaidi katika kipindi hichi ambapo nchi ipo katika uchumi wa kati na kuhakikisha kwamba mwananchi mmoja mmoja anafurahia maisha katika awamu hii ya tano chini ya Rais John, Magufuli” alisema
Aidha Nyamoga alisema kuwa katika sekta ya afya atahakikisha ujenzi wa zahanati ulioanzishwa na wanakijiji cha Nyawegete ndani ya kipindi cha miaka mitano wanakamilisha ili iweze kuhudumia wananchi na kuwapongeza kwa hatua hiyo.
Aliongeza kuwa changamoto ya maji wanayokabiliana nayo wananchi wa kijiji hicho atahakikisha anashirikiana na RUWASA ili kuondoa tatizo hilo na vitongoji 17 ambavyo havijapata huduma ya umeme wanapata huduma hiyo.
Aidha alichangia mifuko 10 ya saruji ili kukamilisha ujenzi wa matundu ya choo katika shule ya msingi Nyawegete na kuendelea kuwaahidi suala la mawasiliano ya simu ili kupata kampuni ambayo itawekeza kata ya Masisiwe ili kuondokana na tatizo la mawasiliano.
Nyamoga ambaye mbunge kwa mara ya kwanza katika jimbo hilo alisema kuwa kwa kushirikiana na wananchi wa kata ya Masisiwe atahakikisha anafanikisha adhama ya wananchi kuwa na jengo la ofisi ya kata ya Masisiwe .
No comments:
Post a Comment