HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 15, 2021

KASEKENYA: ONGEZENI UBUNIFU NA KUZINGATIA MAADILI

Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, akizungumza na uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), (hawapo pichani), wakati wa ziara yake kwa wakala huo, mkoani Dar es Salaam. 

 

Dar es Salaam, Tanzania

 
Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewataka wahandisi, wakandarasi, wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi kuongeza ubunifu na kuzingatia maadili katika majukumu yao ya kazi ili kuliwezesha Taifa kunufaika na thamani ya fedha katika miradi ya ujenzi inayoendelea.
 

Akizungumza mkoani Dar es Salaam, mara baada ya kutembelea taasisi za Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),  Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), amewataka wataalamu hao kufahamu kuwa maendeleo na ukuaji wa uchumi unategemea sana taaluma zao.

"Tumieni fursa za miradi mikubwa inayoendelea nchini kujifunza ili kuliwezesha Taifa kuwa na watalaam wake watakaomudu kujenga miradi mikubwa katika siku zijazo", amesema Naibu Waziri Kasekenya.

Aidha, amezitaka taasisi binafsi na umma kuweka mipango madhubuti ya kuwapokea wanafunzi wa fani za kihandisi katika mazoezi ya vitendo ili kuwajengea uwezo.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Crispianus Ako, amesema TANROADS imejipanga kuhakikisha barabara zote kuu na za mikoa zenye urefu wa KM 36,258 zinapitika katika kipindi chote cha mwaka.

Amesisitiza kuwa katika kuhakikisha barabara zinalindwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu TANROADS inasimamia mizani 82 katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Prof. Ninatubu Lema, amesema bodi hiyo inaendelea kusajili na kusimamia shughuli za kihandisi nchini ambapo zaidi ya wahandisi elfu thelathini (30,000) wamesajiliwa hadi  sasa.

Katika kuhakikisha wahandisi wazingatia maadili, Msajili wa ERB, Mhandisi Patrick Barozi, amesema bodi hiyo imekuwa ikitoa leseni ya uhandisi na imekuwa ikiwachukulia hatua kali wahandisi wanaokiuka maadili.

Mhandisi Barozi ametoa rai kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi ili idadi ya wahandisi wanawake iongezeke ambapo hadi sasa kati ya wahandisi elfu thelathini (30,000) walisojaliwa nchini wanawake ni asilimia 11 tu.

Naye Msajili wa Bodi ya Wakandarasi (CRB), Rhoben Nkori, amemuhakikishia Naibu Waziri Kasekenya kuwa bodi hiyo inaendelea kuhakikisha wakandarasi wazawa wanaongezeka na kupata miradi mingi ili uwekezaji mwingi wanaoufanya uwe wa  hapa nchini.

"Tunahakikisha wakandarasi wazembe wanafutiwa usajili ili wakandarasi waliopo wawe wale wanaofanya kazi kwa ubunifu na uzalendo", amefafanua Nkori.

Kwa upande wa Msajili wa Bodi ya AQRB, Mkadiriaji Majenzi Edwin Nnunduma, amesema kuongezeka kwa idadi wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi kutaboresha sekta ya ujenzi hapa nchini na kuwezesha miradi mingi ya ujenzi kuwa ya uhakika na yenye viwango vya ubora.

Naibu Waziri Kasekenya yupo mkoani Dar es Salaam katika ziara ya kukagua taasisi zilizo chini ya Wizara yake ambapo ametembelea na kuzungumza na uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS),  Bodi ya Usajili wa Wakandarasi (CRB), Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

No comments:

Post a Comment

Pages