Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama (katikati), akifafanua masuala mbalimbali kuhusu wajibu na haki za Walimu, katika mkutano wa pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi Tanzania Bara, Dodoma, Januari 7, 2021.
Na Veronica Simba
Serikali
imewahamasisha Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini,
kujiendeleza kielimu katika ngazi mbalimbali ili kuboresha zaidi
utendaji wao wa kazi.
Wito
huo umetolewa jijini Dodoma leo, Januari 7, 2021 na Kaimu Katibu wa
Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama wakati akizungumza na
Wajumbe wa Mkutano wa Pili wa Umoja wa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi
Tanzania Bara.
Akifafanua,
amesema kuwa, kujiendeleza kielimu ni haki ya msingi kwa watumishi wote
wa umma wakiwemo walimu, ndiyo maana Serikali kupitia Tume imekuwa
ikiwahamasisha kuitumia fursa hiyo ipasavyo.
Chitama
amekemea tabia ya baadhi ya Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Wakuu wa
Shule za Sekondari Tanzania Bara, ambao hukataa kutoa ruhusa kwa
watumishi walio chini yao wenye nia ya kujiendeleza kielimu.
Hata
hivyo, Kaimu Katibu huyo amesisitiza kuwa Walimu wote wa shule za umma
wenye nia ya kujiendeleza kielimu, wanapaswa kuzingatia taratibu
zilizowekwa na Mamlaka ikiwemo kufuata Mpango wa Mafunzo.
Aidha,
amewasisitiza kuhakikisha wanapata ruhusa ya maandishi kutoka kwa Wakuu
wao, kabla ya kwenda masomoni kwani kinyume chake watakabiliwa na
mashtaka ya utoro kazini ambayo adhabu yake ni kufukuzwa kazi.
“Tumekuwa
tukipata rufaa nyingi za kesi za Walimu ambao walitoroka kazini na
kwenda masomoni hivyo kufukuzwa kazi. Serikali inapenda walimu msome
lakini fuateni taratibu zilizowekwa,” amesisitiza.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Ajira na Maendeleo ya Walimu kutoka
TSC, Mecktildis Kapinga, akifafanua kuhusu utaratibu wa kupanda vyeo,
ameueleza Mkutano huo kuwa, kanuni inaelekeza kutompandisha cheo
mtumishi yeyote wa umma akiwa masomoni, hadi pale anapohitimu ndipo
mchakato wa kumpandisha hufanyiwa kazi.
“Naomba
mtambue kuwa utaratibu huo ni kwa watumishi wote wa umma, na siyo kwa
walimu pekee kama ambavyo baadhi yenu mmekuwa mkinung’unika,” amefafanua
Kapinga.
Mkutano huo wa
siku tatu, ulianza Januari 5, 2021 huku ukiongozwa na kaulimbiu isemayo
uongozi na usimamizi makini wa elimu, utaimarisha Tanzania katika uchumi
wa kati.
Tume ya
Utumishi wa Walimu ni Mamlaka ya Ajira na Nidhamu kwa walimu wa shule za
msingi na sekondari Tanzania Bara, walio kwenye utumishi wa umma.
No comments:
Post a Comment