Dk. Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa makubaliano ya uratibu na uandishi wa vitabu 32 vya kiada kwa masomo ya ufundi kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya TET na DIT iliyofanyika Dar es Salaam leo.
Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Janeth Komba na kulia ni Mkuu wa DIT, Profesa Praskids Ndomba wakisaini mkataba huo.
Na Irene Mark
KATIBU Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo amesema Serikali haina mpango wa kuhamisha jukumu la uandishi wa vitabu na uandaaji wa mitaala kutoka kwa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).
Kwa sababu hiyo amewataka waandishi binafsi wa vitabu vya Kiada na Ziada kwa shule za Msingi na Sekondari kushirikiana na TET katika kufanya uandishi bora kwa maslahi ya taifa hili.
Dk. Akwilapo amesema hayo leo Juni 17. 2021 wakati wa haflaa ya utiaji saini wa mkataba wa makubaliano ya uratibu na uandishi wa vitabu 32 vya kiada vya masomo ya ufundi kwa shule za sekondari kati ya TET na Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT).
Hafla hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vya ofisi za TET jijini Dar es Salaam ilihudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk. Aneth Komba, Mkuu wa DIT, Profesa Praksedis Ndomba, wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi wa taasisi hizo na watumishi wa taasisi hizo.
“Jukumu la kuandaa mitaala na kuandika vitabu lipo chini ya TET hili lilikuwa chachu ya uanzishwaji wa taasisi hii lakini likaondolewa mwaka 1992 na hapo sasa waandishi mmoja mmoja wakawa wanaandaa vitabu kwa ajili ya watwoto wetu.
“...Mwaka 2013 lilipotokea tatizo la dosari za vitabu kule bungeni wizara sasa mwaka 2014 ikaamua kurejesha jukumu hilo kwa TET na ndicho kinachoendelea kufanyika.
“Hakuna mpango wa kuliondoa jukumu hili hapa japo tulipingwa sana kwa sababu za kimaslahi basi tuwakaribishe waandishi mmoja mmoja kufika hapa kwa washirikiane na Taasisi yetu hii kuandika vitabu. Hapa kuna wataalam wa hizo kazi,” anasema Dk. Akwilapo.
Amesema ni jambo la kawaida kwa serikali kutumia rasilimali ilizo nazo mahali ambapo rasilimali hizo zipo.
“Kwa mantiki hii, TET watatumia rasilimawatu kutoka DIT kufanikisha malengo yake. DIT nao kupitia ushiriki huu kwenye kazi ya Uandishi wa Vitabu vya Kiada vya Masomo ya Ufundi watakuwa wametekeleza lengo lake la kusaidia jamii,” amesisitiza Dk. Akwilapo.
Akizungumzia mkataba huo, Dk. Komba amesema DIT inaandika vitabu vya masomo ya ufundi kwa kushirikiana na TET kwa kutumia mihutasari iliyoboroshwa mwaka 2019.
“Vitabu hivyo ni vya masomo yote nane ya shule za ufundi ambayo ni Engineering Science, Civil Engineering, Surveying, Architectural Draughting, Building Constraction, Woodwork and Painting, Mechanical Engineering, Electrical Engineering na Electronics and Communication Engineering kwa kidato cha kwanza hadi cha nne.
“Kwa kadiri ya makubaliano yetu kazi hii itaanza Juni 22.2021 na kukamilika kwa siku 160 hivyo tunatarajia kazi ya uchapaji wa vitabu hivyo itaanza Desemba Mosi mwaka huu... vitabu hivyo tunatarajia kuanza kutumika shuleni kuanzia Januari mwaka 2022,” anasema Dk. Komba.
Kwa mujibu wa Dk. Komba uandishi wa vitabu hivyo utahusisha walimu wa masomo ya ufundi kutoka vyuo vingine na wataalam wa ufundi.
Mkuu wa DIT, Profesa Ndomba amesema kazi ya kuandika vitabu 32 kwa masomo 8 ya elimu ya ufundi kwa shule za sekondari imekuja kwa wakati muafaka na kwamba itasaidia katika kuoanisha elimu wanayoipata kutoka ngazi ya sekondari hadi kuingia katika vyuo na Taasisi za ufundi hapa nchini.
“Na hapa nisisitize kuwa kazi hii tutaifanya kwa weledi na umakini mkubwa kwani tunao wataalamu waliobobea katika elimu ya ufundi,” anasema Profesa Ndomba.
No comments:
Post a Comment