Na Lydia Lugakila, Bukoba
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Charles Mbuge amewaapisha rasmi wajumbe wa Baraza la Ardhi na Nyumba wa Wilaya ya Muleba mkoani humo na kuwataka kupambana na mrundikano wa kesi za ardhi zilizodumu tangu mwezi Desemba mwaka 2020.
Hafla hiyo fupi ya kuwaapisha wajumbe hao wa baraza la ardhi na nyumba iliyofanyika katika ukumbi wa mkoa huo ambapo mkuu wa mkoa huo Meja Jenerali Charles Mbuge amesema kuwa wilaya ya Muleba imekuwa na changamoto ya kutokuwa na wajumbe wa baraza la ardhi na nyumba tangu mwezi Desemba 2020, baada ya wajumbe wa waliokuwepo kumaliza muda wao, jambo lililoifanya wilaya hiyo kuwa na mrundikano wa kesi nyingi za migogoro ya ardhi.
Meja Jenerali Mbuge amewasisitiza wajumbe hao kutenda haki katika maamuzi yao, huku akikemea kutojirudia kwa baadhi ya makosa yaliyojitokeza katika kipindi cha nyuma ikiwemo wajumbe wa baraza la ardhi waliopita kujihusisha na vitendo vya kupokea rushwa, kukosa uadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao, kutoa siri ya kile kilichoamuliwa na baraza kabla ya maamuzi kutoka rasmi, kujisifu na kutamba mitaani kwa kujiona wapo juu ya sheria matendo ambayo yamekuwa yakiwasababishia matatizo wenyeviti wa baraza kupata wakati mgumu katika majukumu yao.
" Umri wenu unafaa kabisa tendeni haki Migogoro inadidimiza uchumi wa nchi, tumieni muda mwingi kupunguza kesi mkoa wa Kagera una baadhi ya changamoto hasa mauaji yanayotokana na ardhi na kuwa hatua itachukuliwa kwa wajumbe watakaokiuka taratibu na sheria katika majukumu yenu alisema Meja Jenerali Charles Mbuge
Aidha kwa upande wake jaji mfawidhi mahakama kuu kanda ya Bukoba Dr Ntemi Kileka Majengo amesema kuwa mkoa wa Kagera una kesi nyingi asilimia kubwa zikiwa ni za migogoro ya ardhi na nyumba na kuwa wanapokea rufaa nyingi hivyo kuwaomba wajumbe hao kutanguliza haki na kuondoa upendeleo.
Naye katibu tawala Mkoa wa Kagera Profesa Faustin Kamuzora ameeleza kuwa wilaya ya Muleba ina watu 700, 000 hivyo wajumbe hao wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanatatua migogoro ya ardhi ili kuruhusu wananchi wa mkoa huo kunufaika kiuchumi.
Amesema kuwa ardhi ya mkoa huo ina rutuba nzuri na kuwataka kuachana na kupoteza muda wao, katika kesi zisokuwa na maana huku akiwaomba viongozi wa dini kusaidia kuelimisha jamii kutumia muda mwingi kufanya mambo ya maendeleo kuliko kukaa katika migogoro.
Kwa upande wao viongozi wa dini akiwemo shekhe wa mkoa wa Kagera Haruna Kichwabuta na Askofu Dr Abednego Kesho Mshahara wa Kanisa la kiinjili la kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya kaskazini Magharibi wamewasihi wajumbe hao kutokuwa vyanzo vya kusababisha migogoro kwa wananchi badala yake wawashauri na kutatua Migogoro yao kwa kuzingatie utaratibu ili kupunguza viashiria vinavyosababisha mauaji baada ya migogoro hiyo.
Hata hivyo wajumbe wa baraza la ardhi na nyumba walioapishwa kutoka wilayani Muleba ni pamoja na Georgia Kaijage Machumu, Justus Mutalemwa, Bartholomayo Aloyce Rugaimukamu na Pastory Juvenary ambao pia wameahidi kuteketeza majukumu yao kwa haki bila ubaguzi.
No comments:
Post a Comment