HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 17, 2021

TCRA NA UCSAF WAPEWA MWEZI MMOJA KUJA NA MAPENDEKEZO KUTATUA CHANGAMOTO ZA MWINGILIANO WA MAWASILIANO MIPAKANI


 

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (mwenye suti ya kijivu) akisalimiana na baadhi ya wananchi wa kijiji cha Mtakuja kilichopo Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro wakati wa ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu Kijiji hicho.

 

Na Mwandishi Wetu, HAI

 

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew ametoa mwezi mmoja kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kutoa maelezo ya kinachosababisha mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani  na namna bora ya kutatua changamoto hiyo

 

Mhandisi Kundo amezungumza hayo katika ziara yake ya kukagua ubora wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani alipotembelea Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) kwa upande wa lango la Machame la kupandia mlima huo lililopo Wilayani Hai

 

“TCRA na UCSAF nawapa mwezi mmoja mje na majibu ya kutatua changamoto za mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani ikiwa ni pamoja na maeneo ya hifadhi za Taifa kwa kuwa kuna maeneo ya mipakani kama Namanga minara ipo lakini bado kuna tatizo la mwingiliano wa mawasiliano”, alizungumza Mhandisi Kundo

 

Aliongeza kuwa ni muhimu kujiridhisha kama sababu ni nchi ya Tanzania kutii sheria, kanuni na miongozo ya Shirika la Kimataifa linalosimamia Mawasiliano (ITU) kuhusu uwekaji wa miundombinu ya mawasiliano katika maeneo ya mipakani na hatua zilizochukuliwa za kutatua changamoto hiyo ili nchi jirani nazo zifuate utaratibu uliowekwa na ITU

 

Alisema kuwa eneo la hifadhi ni eneo nyeti sana kwasababu ni maliasili ambayo nchi inajivunia kama kivutio cha Taifa, chanzo cha ukusanyaji wa mapato kutokana na shughuli za utalii na pia ni urithi wa vizazi vijavyo hivyo ni eneo muhimu kuwa na mawasiliano ya uhakika

 

Aidha, katika hatua nyingine Mhandisi Kundo ameutaka uongozi wa hifadhi hiyo kuharakisha mchakato wa utoaji wa vibali vya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi kwa sababu ni moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na watoa huduma kwa kuchelewesha au kukwamisha ujenzi wa minara katika maeneo hayo

 

Naye Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi wa KINAPA Angela Nyaki amesema kuwa wapo tayari kushirikiana na watoa huduma katika  kufanikisha upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi kwa kuharakisha mchakato wa kutoa vibali sambamba na kuwapa watoa huduma maeneo ambayo wanaweza kujenga minara ya mawasiliano bila kuathiri uoto wa asili au viumbe hai vilivyopo katika hifadhi hiyo

 

Ameongeza kuwa watalii wengi wanaofika mahali hapo kwa ajili ya kupanda Mlima Kilimanjaro wamekuwa wakishindwa kutumia huduma ya live streaming wakiwa juu ya mlima  kutokana na mwingiliano wa mawasiliano na mtandao wa Safaricom wa nchini Kenya kitu kinachosababisha watalii kukosa mawasiliano wanapopanda mlima kwasababu simu zao zinakuwa zinasoma mtandao wa nchi jirani.

 

Kwa upande wa Afisa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Albert Richard amesema kumekuwa na malalamiko mengi ya watoa huduma kuhusu ucheleweshaji wa vibali vya ujenzi wa minara ya mawasiliano katika maeneo ya hifadhi za Taifa nchini kitu ambacho kinachangia kwa kiasi kikubwa kwa watoa huduma kuamua kwenda kujenga mnara katika maeneo ambayo hayana changamoto za utoaji wa vibali

 

Aidha, watendaji wa TCRA, UCSAF, KINAPA pamoja na wawakilishi wa Makampuni ya simu nchini wamekiri kupokea maelekezo ya Naibu Waziri na kuahidi kuyafanyia kazi kama alivyoelekeza kwa lengo la kutatua changamoto ya mwingiliano wa mawasiliano  katika maeneo ya mipakani na maeneo ya hifadhi za Taifa nchini

 

Katika ziara hiyo Mhandisi Kundo aliambatana na watendaji kutoka katika taasisi za mawasiliano ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Shirika la Posta Tanzania (TPC) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) pamoja na wawakilishi wa makampuni ya simu ya Vodacom, Tigo, Airtel, TTCL, Halotel na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai kwa lengo la kukagua ujenzi, ubora, uwezo na upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya mipakani.


No comments:

Post a Comment

Pages