HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 06, 2021

Wabunifu NMNA waja na teknolojia kuongeza kipato



Mbunifu Gofrey Kasembe  kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), akielezea mashine aliyobuni ambayo inaweza kumwagilia shamba bila mkulima kuwepo shambani.


Mbunifu Jonas Katial kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), akielezea mashine aliyobuni ambayo inaweza kumwagilia shamba bila mkulima kuwepo shambani.

 

Na Selemani Msuya

 

WABUNIFU Jonas Katial na Gofrey Kasembe kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA), wamebuni mashine mbili tofauti ambazo hazihitaji mtumiaji kuwepo eneo la tukio kutoa huduma bali teknolojia ndio itaweza utoaji huduma.

Akizungumzia ubunifu wake Katial alisema yeye amebuni kifaa ambacho kinatumika kumwagilia shamba bila mkulima kuwepo katika shamba husika jambo ambalo linachochea mkulima kujihusisha na shughuli nyingine za uzalishaji.

Katial alisema mashine hiyo inafanya kazi baada ya kupima hali ya udongo ambapo ukifungwa katika eneo la shamba mashine itawasha mota na pampu ya maji kusukuma maji kwenye shamba ambapo muda wote huo taa ya kijani itakuwa inawaka na pale ambapo shamba linamwagiliwa maji lote taa nyekundu inawaka na kuacha kumwaga maji.

“Mfumo huu wa kumwagilia maji kwa teknolojia (Outomatic), unaunganishwa na simu ya mwenye shamba ambao atatumiwa ujumbe wa meseji kuwa moto inawaka na shamba linamwagiliwa na pale ambapo shamba limemwagiliwa ujumbe mfupi utakuja kwa mkulima kumuambia tayari shamba limemwagiliwa lote,” alisema.

Alisema mfumo huo utarahisisha wakulima kufanya kazi mbili au tatu kwa wakati mmoja na kuondokana na utamaduni wa wakulima kukaa shamba muda wote.

Mbunifu huyo alitoa rai kwa serikali na wadau wengine kuwawezesha ili aweze kuboresha ubunifu wake na kusambaza kwa wakulima nchini kote ili kuchochea shughuli za maendeleo na uchumi.

Kwa upande wake Mbunifu Kasembe alisema yeye amebuni mashine ambayo inauza maji bila mwenye bomba ya kuuza maji kuwepo.

Kasembe alisema kwa utaratibu wa sasa wauza maji wanajikita katika shughuli moja ya kuuza maji jambo ambalo linawapotezea muda.

Alisema pia maeneo mengi usiku maji hayapatikani kwa kuwa wauza maji wamelala lakini ujio wa mashine hiyo utaruhusu maji kuuzwa saa 24 hali ambayo itaongeza kipato na kuokoa muda kwa muuzaji.

“Hii mashine imetengenezwa katika mfumo ambao unaweza kuuza maji kulingana na kiwango cha fedha yako, lakini pia hahitaji muuzaji awepo katika eneo la kuuzia maji, bali yeye atakuja kukusanya fedha zake kinachihitajika ni umeme kuwepo,” alisema.

Alisema ubunifu wao wote umejikita katika kutatua changamoto za watu kupoteza muda katika eneo moja jambo ambalo linakwamisha shughuli za maendeleo na uchumi.

No comments:

Post a Comment

Pages