HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 06, 2021

WAZIRI PROF.NDALICHAKO AFURAHISHWA NA MBINU ZA CHUO KIKUU MZUMBE KUTATUA CHANGAMOTO YA AJIRA

 

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof.Lughano Kusiluka akimkaribisha katika banda la Chuo Kikuu Mzumbe Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Prof. Joyce Ndalichako (mwenye nguo ya bluu) alipowasili bandani hapo. 


Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chuo Kikuu Mzumbe. Bi. Rose Joseph akiutambulisha mradi wa ufugaji Samaki na kilimo cha mbogamboga uliobuniwa na Mwanafunzi Nelson Kisanga (mwenye tisheti ya njano kushoto) kwa Mhe. Waziri Ndalichako.
Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe ndaki ya Mbeya Ezekiel Wellia akielezea  kiungo cha chai Tiba  alichokitengeneza kwa mbegu ya parachichi.


Mwanafunzi Ezekiel Blassio akimwelezea Waziri hatua za upimaji maji  ambao ni mradi wa huduma kwa jamii unaotekelezwa na Chuo kikuu Mzumbe kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Antwerp cha nchini Ubelgiji, kuwezesha jamii kutambua ubora wa maji kwenye vyanzo halisi ili  kuimarisha afya.
 


Waziri Prof.Ndalichako akisikiliza maelezo kuhusu huduma ya msaada wa sheria inayotolewa bure katika maonesho hayo kupitia kituo chake cha msaada wa Sheria ambacho hutoa huduma hiyo kwa jamii zinazozunguka Chuo hicho mkoani Morogoro.

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Joyce Ndalichako ametembelea banda la Chuo Kikuu Mzumbe katika maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam, na kufurahishwa na jinsi Chuo hicho kinavyotumia Wataalam wake kuisaidia Jamii kukabiliana na changamoto ya ajira na mbinu za biashara. 

Akiwa bandani hapo Prof.Ndalichako amejionea mafanikio ya andiko la mradi wa kutengeneza ajira 200,000 katika mkoa wa Songwe, lililofanywa na chuo hicho ukilenga ujenzi wa kiwanda cha chumvi utakaogharimu shilingi bilioni 41.

Akieleza namna chuo hicho kilivyoshiriki kufanikisha mpango huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. Lughano Kusiluka  amesema hatua ya chuo hicho kuamua kusaidia Mkoa wa Songwe imetokana na makubaliano yaliyofikiwa na uongozi wa Mkoa huo kuongeza mashirikiano na kutumia wataalamu wa Chuo Kikuu Mzumbe kufikia malengo ya maendeleo waliyojiwekea.

Akikagua shughuli nyingine zinaoonyeshwa kwenye banda hilo, Waziri Ndalichako amevutiwa na namna Chuo kinavyowaandaa, kuwaongoza na kuwawezesha Wanafunzi wa fani zote kubuni miradi ya biashara, ujasiriamali na teknolojia inayotatua changamoto mbalimbali katika jamii .

Waziri Ndalichako ameshuhudia bunifu mbalimbali za wanafunzi, pamoja na teknolojia ya ufugaji wa samaki na kilimo cha mbogamboga kwa kutumia mvuke, teknolojia ya kutengeneza gundi kali kwa kutumia takataka, kiungo cha chai tiba iliyotengenezwa kwa mbegu ya parachichi, mifumo ya kielektoniki  ya kufuatilia afya ya mama mjamzito na mtoto, teknolojia ya kuzuia matukio ya uvunjaji wa sheria za barabarani, pamoja na teknolojia ya kulinda ubora na kudhibiti upotevu wa bidhaa zinazozalishwa viwandani.

No comments:

Post a Comment

Pages