Na Mwandishi Wetu
KATIKA kudhihirisha ubora na upekee wa Benki ya NMB, kwa mwaka huu imeshinda tuzo nne za kimataifa zote zikiitaja kuwa Benki bora zaidi Tanzania.
Ambapo tuzo hizi zinafanya jumla ya tuzo zote ambazo NMB imezipata mwaka 2021, kufikia sita.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Bi Ruth Zaipuna alisema kupata tuzo hizo zinatokana na sababu kuwa NMB ni benki rafiki kwa wateja wake.
Tuzo hizo ni pamoja na Tuzo ya Benki Bora ya Biashara na Benki Bora ya Huduma za Uwekezaji Tanzania mwaka 2021 zote kutoka Jarida la World Economic Banking, tuzo ya Benki Bora kwa Ubunifu wa Huduma za Wateja Binafsi kutoka Jarida la International Banker na tuzo ya Benki Bora ya Wateja Binafsi kutoka Jarida la International Business.
“Tuzo hizi zinaendana na dira yetu ya kuifanya NMB kuwa benki bora zaidi Tanzania, sote tufahamu kuwa tuzo hizi ni za kimataifa zimetolewa na majarida yanayoaminiwa na taasisi za kifedha duniani, hivyo zimezingatia vigezo, ufanisi na utendaji wetu,” alisema Bi Zaipuna.
Itakumbukwa mapema mwaka huu, Benki ya NMB ilitajwa kwa mara ya tisa mfululizo kuwa Benki bora zaidi Tanzania na Jarida la kimataifa la Euromoney na Benki bora ya wateja Binafsi kutoka Jarida la Global Banking and Finance. Hizi ni tuzo za juu kabisa za ubora zinazotolewa na majarida makubwa duniani yenye makao yake makuu jijini London na nchini Marekani.
Katika maelezo yake kwa wanahabari, Bi Zaipuna alisema tuzo hizo zimetolewa kwa kuzingatia vigezo kadhaa kwa benki vilivyopendekezwa vya ufanisi wa mahesabu na utendaji kwa ujumla, mkakati wa huduma za kidijitali, huduma jumuishi za fedha, usalama wa huduma za kimtandao na uwajibikaji wa benki katika jamii inayoizunguka. Leo hii, zaidi ya asilimia 93 ya miamala yote ya benki ya NMB inafanyika nje ya matawi ya benki.
Vigezo vingine vilivyotumika ni mtaji wa benki, mapato yatokanayo na mali za kampuni, uwiano wa fedha na gharama za uendeshaji, kiwango cha amana za wateja, Kiwango cha Mikopo katika soko, Uwiano kati ya mikopo na amana za wateja, uwiano wa mikopo isiyolipika, na uwiano wa hasara itokanayo na mikopo isiyolipika.
“Tuzo hizi zinadhihirisha nafasi ya uongozi wa Benki ya NMB katika sekta ya kibenki nchini. Jopo la majaji wa tuzo zote nne waliona kuwa huduma za kidigitali na za uwakala pamoja na mchango wa benki katika jamii, zimechangia katika ushindi huo,” alisema Bi Zaipua na kuongeza:
“Tunaendelea kuwekeza katika tekinolojia na mtandao wetu wa matawi kwa makini sana na kuongeza nguvu kwenye ubunifu ili kuendelea kutoa suluhishi bora za huduma sokoni.”
Kwa miezi 12 iliyopita, Bi Zaipuna alisema “Benki imeendelea kuboresha huduma zake ili kufikia mahitaji ya wateja, hivyo kuziba pengo la huduma na suluhishi za kifedha sokoni.”
Bi Zaipuna alisema kuwa uwekezaji wa teknolojia umechangia kupanua wigo wa mtandao wake na kurahisisha ukamilishaji wa miamala hivyo kuboresha zaidi Huduma kwa wateja.
NMB imeendelea kuleta matokeo chanya kwa jamii za kitanzania kwa kuleta huduma zenye ubunifu wa hali ya juu na kuiweka jamii karibu zaidi kwa Benki hususan baada ya uzinduzi wa asasi ya kiraia ya NMB Foundation na Mpango wa Ufadhili wa masomo wa Nuru Yangu Scholarship and Mentorship Program kwa watoto wenye ufaulu wa juu kutoka kaya masikini.
No comments:
Post a Comment