HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 16, 2021

Bilioni 46.4 zatumika kuchapa vitabu vya kiada

 


Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania Dkt. Aneth Komba akizungumza  wakati wa uzinduzi wa kazi ya usambazaji wa vitabu vya kiada vya shule ya msingi na sekondari jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI  Mkuu wa Taasisi ya elimu Tanzania (TE) Dk. Aneth Komba, amesema sh Bilioni 46.476  zimetumika katika kuchapa vitabu vya kiada  nakala 20.9 vya elimu kuanzia ngazi ya Awali, Msingi, Sekondari.


Vitabu hivyo ni vya michepuo ya Kiswahili na Kiingereza kwa masomo yote, pia  vipo vya nukta nundu na vitabu kwa ajili ya wanafunzi wa awali na vitabu vya wanafunzi walio nje ya mfumo rasmi.

Hayo ameyasema leo jijini Dar es Salaam, katika uzinduzi wa zoezi la usambazaji wa vitabu hivyo katika halmashauri zote 184 nchini kwa uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili.


Dk Komba,  alitaja makundi ya vitabu vinavyoandaliwa kuwa ni vitabu vya kiada vya masomo yote ya madarasa ya Awali, Darasa la I-IV kwa shule zinazotumia lugha ya kingereza na kiswahili kufundishia, viongozi vya mwalimu I-VII, Mihtasari, viongozi vya mwalimu na vitabu vya wanafunzi walio nje ya mfumo rasmi kundirika la I mwaka wa I na wa II na vitabu vya kiada kidato cha I-IV


Kwa upande wa Sekondari vitabu vilivyoandaliwa ni kwa masomo ya Bailojia, Fizikia, Home Economics, Kiswahili, Civics, Kemia, ICs Mathematics, Jiografia, Historia, kingereza na Kilimo.


Alisema vitabu hivyo vimeandaliwa na wataalamu wa TET kwa kushirikiana na wataalamu wengine kutoka vyuo vikuu, vyuo vya Ualimu pamoja na walimu kutoka shule za Sekondari na Msingi


Kwa upande wa Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia , Profesa Joyce Ndalichako, amewaagiza maafisa elimu wote wa ngazi za halmashauri kuhakiksha wanasimamia  usambazaji wa vitabu hivyo ili vifike mashuleni  kwa wakati na kutumika.


Alisema lengo ya Serikali ni kuwapatia elimu bora watoto wa kitanzania na kwamba  mtoto akisoma na kuandika ndo msingi.


“Hatutaki kuona mtoto anaingia darasa la tatu  hajui kusoma wala kuandika,” alisema Ndalichako.


Alisema vitabu vya kiada ni nyenzo muhimu katika kutekeleza dhana nzima ya ufundishaji na ujifunzaji kwani humrahisishia mwanafunzi kuweza kufuatilia yale yanayofundishwa, kujisomea wenyewe lakini pia yanamuongoza mwalimu katika utekelezaji wa jukumu zima la ufundishaji.


Aidha amemshukuru mkuu wa majeshi ya ulinzi na usalama Jenerali Venance Mabeyo kwa kuendela kutoa ushirikiano kwa Wizara anayoisimamia katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo la kutoa magari kwa ajili ya usambazaji wa vitabu vya kiada kwa shule ya Msingi na sekondari.


Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dk Leonard Akwilapo, alisemaa wizara itaendelea kuisaidia Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) ambayo iko chini ya Wizara ili kuhakikisha inatekeleza majukumu kwa ufanisi kwani inasimamia majukumu yote kuandaa mitaala, mihtasari katika ngazi ya elimumsingi.


Nae Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Gerald Mweli, amemuahidi Waziri Ndalichako kuwa Vitabu hivyo pindi vitakapofika katika Halmashauri watahakikisha ndani ya wiki moja viwe vimefika shuleni na kuanza kutumika ili kutofifisha juhudi za Rais za kuhakikisha watoto wa kitanzania wanapata elimu iliyo bora.

No comments:

Post a Comment

Pages